Taasisi ya HakiElimu yatoa mapendekezo matano kwa Serikali

New Content Item (2)

Mkurugenzi Mtendaji, Dk John Kalage aliyekaa katikati akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani,  jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Kuelekea upangaji wa bajeti ya sekta ya elimu HakiElimu imetoa mapendekezo matano katika uzingatiwaji wa vipaumbele ili kuleta ufanisi katika utoaji wa elimu.

Dar es Salaam. Taasisi ya HakiElimu imetoa mapendekezo matano kwa Serikali inapoelekea katika upangaji wa bajeti ya sekta ya elimu kwa mwaka wa fedha 2024/25  ambayo ni  kuhusu bajeti ya uajiri na mafunzo ya walimu, walimu wa ufundishaji Tahasusi mpya,uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya kiada,ujumuishi wa teknolojia wa mtaala mpya na marekebisho ya sheria ya elimu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Aprili 23, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dk John Kalage amesema kuelekea bajeti hiyo ya mwaka wa fedha 2024/25 wametoa mapendekezo matano kwa ajili ya uzingatiwaji wa vipaumbele ili kuleta ufanisi katika utoaji elimu.

"Serikali inapoelekea kwenye bajeti inapaswa kuzingatia mambo makuu mawili ambayo ni utengenezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa (NDV) 2050 na utekelezaji wa mitaala na sera mpya ya elimu 2023 ili kuleta ufanisi katika utoaji wa elimu,"amesema Dk Kalage.

Amesema mapendekezo katika mtaala mpya umekuja na majukumu ya ziada kwa walimu wa ngazi zote, msingi na sekondari ambayo ni wazi ili kuleta ufanisi wa utekelezaji wa mtaala mpya walimu wote wanapaswa kujengewa uwezo wa namna bora ya utekelezaji wake.

kwa mujibu wa taarifa kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ya Novemba 2023, walimu 4,900 kutoka mikoa ya Iringa 1,832, Mwanza 2,100 na Dar es Salaam na Pwani 1,110 walitarajiwa kupata mafunzo ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu ya awali na msingi ulioanza rasmi Januari 2024.

Hata hivyo,amesema idadi hiyo ni ndogo ikilinganisha na idadi ya walimu wa shule msingi ambao jumla yao ni 197,919 shule za umma wakiwa ni 171,993 wakati shule za binafsi ni 25,926.

"Tunapendekeza serikali itenge bajeti ya kutosha ili kuwapatia walimu wengi zaidi mafunzo ya Mtaala mpya ili kuwezesha utekelezaji wa ufanisi.

Pia amesema Serikali ije na mpango maalumu utakaonyesha awamu za utekelezaji wa mtaala mpya hadi kufikia shule zote ambapo shule 96 tu zimepewa idhini ya utekelezaji ikiwa  28 za umma na 68 za binafsi ambapo walimu kutoka shule hizo ndiyo waliopatiwa mafunzo.

"Hata hivyo tunaona kuwa idadi hii ambayo ni asalimia 1.8 ni ndogo ukilinganisha na idadi ya shule za sekondari nchini ambazo ni 5,289 ambapo shule 4,002 sawa na asilimia 75.7 ni za umma na shule 1,287  za binafsi sawa na asilimia 24.3,"amesema.

Amesema hadi Februari 2023 mahitaji ya walimu kwa shule za sekondari ilikuwa 174,632 na waliopo ni 84,700 upungufu ni 89,932 sawa na asilimia 51.5 hivyo Serikali inatakiwa kutoa mafunzo kazini na kuajiri waalimu ili kusaidia utekelezaji wa tahasusi.

Kuhusu usambazaji wa vitabu vya kiada amesema kuwe na bajeti maalumu kwa ajili ya uchapaji na usambazaji wa vitabu mashuleni kwa kuzingatia vitabu hivyo ni vipya na shule hazina akiba mbadala.

"Serikali inatakiwa kuweka mpango maalumu wa usambazaji wa vitabu hivi mashuleni ukianisha muda mahususi wa ukamilishaji wa zoezi hili.mpango huu utasaidia shule ,walimu na jamii kujipanga katika masomo ambayo Serikali itachelewa kuyafikia,"amesema Kalage.

Dk Kalage amezungumzia kuhusu ujumuishi wa teknolojia katika utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu kwa kuwa mtaala huu ni chombo cha kulipeleka Taifa kuelekea mwaka 2050 ni lazima mipango ya utekelezaji uoneshe  kuchagiza matumizi ya teknolojia kuanzia ngazi ya chini.

Akitolea mfano kwa mujibu wa ripoti ya BEST mwaka 2022 inayotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) shule za umma 7,492 sawa na asilimia 45 ya shule zote za umma ndizo zilizokuwa zimeunganishwa na umeme kama nyenzo muhimu katika matumizi ya teknolojia.

Amesema BEST walitoa ripoti ya vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano vilivyokuwepo shule za sekondari za umma ni kompyuta 30,113 ikiwa kompyuta mpakato ni 10,050  ambazo zilitarajiwa kuhudumia wanafunzi 2,671,927.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Dk Kalage amesema ipangwe bajeti kwa ajili ya marekebisho ya sheria ya elimu ya mwaka 2002 na utekelezaji wa mpango wa nne wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP IV) kwani mpango wa tatu na sheria ya elimu ya mwaka 1978 iliyofanyiwa marekebisho haiakisi mabadiliko ya kimuundo na kimfumo.

"Wakati sera mpya ya elimu ya mwaka 2023 inatamka kuwa elimu ya msingi itatolewa kwa madarasa sita sheria ya elimu bado inaonyesha muundo wa miaka saba tofauti inayoleta mkanganyiko katika utekelezaji,"amesema.

Naye,Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Uchechemuzi Mwemezi Makumba amesema wamekuwa wakishauri Serikali kufikia asilimia 20 wa uwekezaji wa bajeti ya sekta ya elimu kwa mujibu wa makubaliano  na sera ya kimataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara.

"Kwa kipindi cha miaka ya nyuma Serikali ilikuwa inakaribia kwenye asilimia hizo kutokana na uhaba wa bajeti lakini kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita uwekezaji umekuwa asilimia 13 hadi 14 na haujapanda kutoka hapo,"amesema Makumba.

Amesema wamekuja na hoja ya mpango wa maendeleo ya elimu ambao umetoa makadirio ya fedha inayohitajika na kuwekezwa inakaribia asilimia 17 hadi 18 kwa fedha inayotakiwa kuwekezwa