Taasisi yazindua mpango mkakati kudhibiti ubora wa elimu

Muktasari:

  • Taasisi ya Regional Education Learning Initiative (Reli) imezindua mpango mkakati wake wa kwanza wa miaka mitatu unaolenga kuangazia changamoto zinazosababisha baadhi ya watoto kushindwa kupata elimu pamoja na ubora wa elimu unaotolewa shuleni.

Dar es Salaam. Taasisi ya Regional Education Learning Initiative (Reli) imezindua mpango mkakati wake wa kwanza wa miaka mitatu uliolenga kuangazia masuala mbalimbali ambayo bado ni changamoto katika upatikanaji wa elimu bora na yenye usawa nchini.

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na baadhi ya watoto kushindwa kupata elimu ambayo ni moja kati ya haki ya msingi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mpango mkakati huo leo Septemba 27, 2023 jijini Dar es Salaam, kiongozi wa taasisi hiyo kwa upande wa Tanzania, Kadija Shariff amesema kwa hapa nchini takwimu zinaonyesha kuwa watoto takribani milioni tatu ambao hawapati elimu kutokana na sababu mbalimbali kati ya hao milioni 1.2 wenye umri kati ya miaka 7-17  hawajawahi kabisa kupata elimu na milioni mbili wakiwa wameacha shule.

"Mkakati huu unaenda kuziangazia kwa kina changamoto ambazo zinawapelekea watoto hao kushindwa kupata elimu na kuja na suluhu," amesema.

Amesema pia mkakati huo umelenga kuangalia ubora wa elimu inayotolewa shuleni na namna ya kuwezesha walimu kutumia mbinu rafiki ambazo zitawawezesha watoto kujifunza vyema.

"Hata malengo ya mtaala uliotengenezwa ni kutengeneza wahitimu ambao ni wabunifu, wenye uwezo wa kutatua matatizo mbalimbali kupitia elimu walioipata hayo yanawezekana kufikiwa ikiwa ubora wa elimu inayotolewa mashuleni itazingatiwa," amesema.

Kiongozi wa Reli nchini Kenya, Samweli amesema baadhi ya changamoto za elimu katika nchi za Afrika Mashariki.

Akitolea mfano changamoto ya baadhi ya watoto kukosa elimu ambayo ilianishwa katika mkutano huo kuwa inaikabili pia nchi ya Kenya.

Changamoto zingine alizobainisha ni pamoja na uhaba wa walimu pamoja na upatikanaji wa miundombinu wezeshi.

"Mambo hayo hupelekea kudorola kwa ubora wa elimu hivyo kushindwa kuzalisha mhitimu ambaye anaendana na hali halisi ya sasa," anasema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tuangoma, Wande Mkonyi ambaye alikuwa ni mgeni rasmi wa hafla hiyo amesema kwa uzoefu wake wa kufundisha watoto wenye mahitaji maalum kwa takribani miaka 28 kuna changamoto mbalimbali zinazokumba wanafunzi katika kundi hilo ikiwemo kukosa mahitaji muhimu ikiwemo chakula, upungufu wa vifaa vya kujifunzia, uhaba wa walimu, changamoto za kimatibabu pale wanapoumwa.

Anasema changamoto hizo zinaleta athari mbalimbali katika ubora wa elimu inayotolewa kwa watoto wenye changamoto hizo.

Hivyo alitoa wito kwa Serikali na mashirika mbalimbali ya elimu kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi kwa wanafunzi hao wenye mahitaji maalumu kujifunza na kuangaliwa utaratibu wa kuwapatia bima ya afya ili kuwapa urahisi wa kupata matibabu pindi wanapopata changamoto za kiafya.