Taha yawezesha upatikanaji wa soko la ndizi Kenya

Muktasari:

  • Asasi ya kilele inayojishughulisha na kilimo cha  mbogamboga, matunda na mimea itokanayo na mizizi na viungo Tanzania Horticultural Association (Taha) imemewezesha upatikanaji wa soko la ndizi nchini Kenya.

Hai. Asasi ya kilele inayojishughulisha na kilimo cha  mbogamboga, matunda na mimea itokanayo na mizizi na viungo Tanzania Horticultural Association (Taha) imemewezesha upatikanaji wa soko la ndizi nchini Kenya.

Kampuni ya Twiga Food kutoka nchini Kenya ndiyo itakayokuwa ikinunua ndizi nchini Tanzania  kwa mkulima wa kampuni ya MackJaro ambaye atakuwa anachukua tani nane kila wiki.

 Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Oktoba 5, 2021 na Meneja Mazingira Wezeshi asasi hiyo ,Kelvin Remen alipokuwa akizungumzia fursa zilizopatikana baada ya kukamilika kwa mkutano wa wadau wa ndizi Kanda ya Kaskazini uliofanyika Septemba 25 mwaka huu na kuongozwa na Waziri wa kilimo , Profesa Adolf Mkenda.

"Katika mkutano huo walishiriki na wadau mbalimbali tuliweka   mikakati ya pamoja  katika kuwahamasisha wakulima kwa kuwajengea uwezo na kuwapa miundombinu stahiki ili waweze kuzalisha na kuwauzia wanunuzi bidhaa hiyo sasa milango imeanza kufunguka," amesema.

Meneja huyo amesema asasi hiyo inalo jukumu la kuwatafutia masoko ya ndani na kimataifa wakulima wa mazao ya horticulture na kuweka jitihada za kuhakikisha uzalishaji unaongezeka na kuleta tija kwa jamii.

"Taha tunawafungulia fursa ya masoko ya bidhaa wanazozalisha wakulima kuanzia masoko ya ndani ,kikanda na Kimataifa, tuataendelea kuhakikisha wateja wanakuja kununua mazao hapa nchini Tanzania," amesema Remen.

Remen amesema fursa hiyo haishii kwa wazalishaji wakubwa tu bali inaenda kwa wazalishaji wadogo wa zao hilo kutoka maeneo mbalimbali wanaozalisha ndizi na hivi sasa wanawasiliana na halmashauri kutekeleza waliyoazimia.

Kwa upande wake Meneja wa uzalishaji wa kampuni ya Mackjaro,Victor Mushi mwenye shamba la ndizi la hekta 143 amesema kutokana na kupatikana kwa soko hilo ana uhakika wafanyakazi  145  alionao wataendelea na ajira zao baada ya fursa ya kusafirisha bidhaa zao nje ya nchi kupatikana.

"Pamoja na kupata mteja huyo kutoka Kenya pia tuna masoko ya ndani ambapo tulikuwa tunauza Dodoma na Dar es Salaam lakini hivi sasa tutaongeza uzalishaji baada ya kupata soko la uhakika,"amesema Mushi.

Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo walisema upatikanaji  wa soko hilo la uhakika unawahakikishi usalama wa ajira zao na kukuza pato la taifa.