Takukuru: Baadhi ya abiria SGR hawalipi nauli sahihi

Muktasari:
- Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Morogoro imegundua baadhi ya abiria wanaotumia treni ya SGR hawalipi nauli sahihi kulingana na safari wanazofanya.
Morogoro. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Morogoro imebaini uwepo wa abiria wachache wanaotumia treni ya SGR ambao hawalipi nauli sahihi ya vituo wanavyoshukia.
Takukuru imesema vitendo hivo, endapo vitaendelea, vitasababisha Shirika la Reli Tanzania (TRC) kushindwa kujiendesha kwa siku zijazo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 15, 2024, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga amesema uchunguzi uliofanyika umethibitisha kuwa baadhi ya abiria wanaotoka Dar es Salaam, hasa wale wanaolipa nauli za kuishia vituo vya jirani, hushindwa kushuka katika vituo vyao na badala yake wanaendelea na safari bila kulipia.

Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Picha na Lydia mollel
"Takukuru imefanya uchunguzi uliothibitisha kuwa baadhi ya abiria wasio waaminifu wanaotokea Dar es Salaam kwenda maeneo mengine, hasa wale wanaolipa nauli za kuishia vituo vya njiani kama vile Pugu (Sh1, 000), Soga (Sh4,000), Ruvu (Sh5,000) na Ngerengere (Sh9,000), hushukia Morogoro. Hali hii inasababisha shirika kupata hasara," amesema Mwakajinga.
Mwakajinga ameongeza kuwa wamefanya kikao na uongozi wa Shirika la Reli ambao walikiri kuwepo kwa hali hiyo na kuahidi kuweka utaratibu wa ukaguzi wa tiketi za abiria pamoja na kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika.
"Uongozi huo umehaidi kuweka utaratibu wa ukaguzi wa tiketi na kuchukua hatua kali dhidi ya abiria yeyote atakayebainika, ikiwa ni pamoja na kuwataka kulipa faini mara mbili ya nauli waliyopaswa kulipa," amesema Mwakajinga.
Hivyo, Takukuru imetoa rai kwa abiria wanaosafiri kwa kutumia treni ya mwendokasi kuwa waaminifu na kulipa nauli ambazo zinakubaliana na safari wanayofanya ili shirika litoe huduma iliyokusudiwa.
Aklizungumzia hilo, Neema George ambaye ni mkazi wa Mazimbu Road, mkoani Morogoro, amesema ni muhimu kwa wananchi kutambua usalama na ufanisi wa huduma za treni kwani uendeshaji wake unategemea kwa kiasi kikubwa mapato yanayotokana na nauli wanayolipa.
"Wanaofanya hivyo wanasahau ufanisi wa huduma wanazopata ndani ya treni na kuwa treni hiyohiyo inatumia nauli wanazolipa kujiendesha.
“Kutolipa nauli halali ni kinyume cha sheria na kunaleta athari kwa uchumi wa shirika, jambo ambalo linaweza kuathiri huduma zinazotolewa kwa abiria wote, hivyo basi kila mmoja anapaswa kuwa mwaminifu na kulipa nauli stahiki ili kuhakikisha kuwa huduma za treni zinaendelea kuwa bora kwa faida kwa jamii yote," ameshauri George.
Nicholas Jerome, mkazi wa Kwachambo mkoani Morogoro, amesisitiza kwamba wanaohujumu malipo ya treni hiyo waache mara moja kwani huduma hiyo imetengeneza ajira kwa vijana wengi.
"Treni ya SGR imeleta ajira kwa vijana wengi lakini pia akina mama wanaojishughulisha na mama lishe. Endapo huduma hii itashindwa kujiendesha kwa sababu ya watu wachache wasio waaminifu, itasababisha wengine kukosa kipato. Hivyo, Serikali ikiwakamata iwachukulie hatua stahiki. Tunafaidika sote," amesema Jerome.