Takukuru yamburuta kortini wakili kwa tuhuma za rushwa

Takukuru yamburuta kortini wakili kwa tuhuma za rushwa

Muktasari:

  • Wakili wa Kujitegemea, Emmanuel Mlaki alifikishwa mahakamani mjini Moshi leo Aprili 8,2021 akidaiwa kupokea fedha hizo kutoka kwa mteja wake akidai zingetumika kumshawishi hakimu awape upendeleo.

Moshi. Madai ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh300,000 kutoka kwa mteja wake, yamemfikisha mahakamani Wakili wa Kujitegemea wa Mjini Moshi, Emannuel Mlaki akikabiliwa na shtaka la kuomba na kupokea rushwa hiyo.

Wakili huyo alifikishwa mahakamani leo Aprili 8,2021  na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Kilimanjaro mbele ya Hakimu Mkazi wa Moshi, Pamela Mazengo na kukana mashtaka yake.

Mlaki ametakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh5 milioni.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Takukuru Kilimanjaro, Frida Wikesi inasema wakili huyo alikamatwa Machi 9,2021 na leo amefunguliwa kesi ya jinai namba 13/2021 katika mahakama hiyo.

Akimsomea mashtaka, wakili wa Serikali anayeshirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS),Furahini Kibanga alidai kati ya Machi 4 na 9, 2021 wakili huyo aliomba fedha hizo akidai zingetumika kama kishawishi kwa hakimu.

Wakili Furahini alidai wakili Mlaki alimwambia mteja wake kuwa fedha hizo zingetumika kumshawishi mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba  Moshi kuharakisha usikilizaji wa shauri lake namba 07/2020 na kumpa upendeleo.