Tamisemi yaomba Sh10 trilioni ikitaja vipaumbele saba

Muktasari:

  • Vipo vipaumbele vya ukusanyaji mapato, kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024, kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya afya ya msingi, elimu msingi na sekondari na kujenga vituo vipya vya polisi.

Dodoma. Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imeliomba Bunge likubali kuidhinisha Sh10.1 trilioni ambazo ni makadirio ya mapato na mtumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25, ikiwa na vipaumbele saba.

Fedha hizo ni ongezeko la Sh981 bilioni ikilinganishwa na fedha zilizoombwa na wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24, kiasi cha Sh9.1 trilioni.

Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa ametoa maombi hayo bungeni leo Jumanne Aprili 16, 2024 wakati akisoma makadirio ya mapato na mtumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25, yanayohusisha mafungu ya Tamisemi, Tume ya Utumishi wa Walimu na mikoa inayojumuisha halmashauri 184.

Mchengerwa amesema fedha hizo zinahusisha Sh3.415 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo kati ya hizo Sh2.2 trilioni ni fedha za ndani na Sh1.1 trilioni ni za nje.

Fedha hizo ni pungufu ya Sh70.7 bilioni, ikilinganishwa na fedha za miradi ya maendeleo zilizoombwa mwaka wa fedha uliopita ambazo zilikuwa Sh3.485 trilioni.

“Katika mwaka 2024/25, Ofisi ya Rais - Tamisemi, taasisi zilizo chini yake, mikoa 26 ikijumuisha halmashauri 184 inaomba idhini ya kukusanya maduhuli na mapato ya ndani ya Sh1.6 trilioni,” amesema.

Mchengerwa pia ametaja vipaumbele saba vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, amewaelekeza wakuu wa mikoa kuwasimamia wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za mitaa kuzingatia vipaumbele vifuatavyo:

“Kuhakikisha ukusanyaji wa mapato uliolengwa unafikiwa kwa asilimia 100 ikiwemo ukusanyaji wa kodi za majengo, kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024 na kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya afya ya msingi, elimu msingi na sekondari kulingana na mipango iliyowekwa,” amesema.

Mchengerwa ametaja vipaumbele vingine ni kuimarisha vyanzo vikuu vya mapato kwa ajili ya kuchachua uchumi kama ilivyobainishwa katika mpango na bajeti wa halmashauri husika.

Pia, amesema viongozi hao wa mikoa wanatakiwa kujenga vituo vipya vya polisi kata 12 na kukamilisha ujenzi wa vituo vya polisi kata 77.

“Kukamilisha ujenzi wa ofisi za vijiji/mitaa angalau tano kwa kila halmashauri na kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga shule za maadilisho zitakazojengwa katika kila mkoa shule moja,” amesema.

Ukusanyaji maduhuli

Mchengerwa amesema katika mwaka 2023/24, taasisi zilizo chini ya Tamisemi, mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa ziliidhinishiwa kukusanya maduhuli na mapato ya ndani ya Sh1.19 trilioni ikilinganishwa na Sh1.07 trilioni iliyoidhinishwa mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la Sh127.55 bilioni, sawa na asilimia 11.90.

“Kati ya fedha hizo, Sh55.14 bilioni ni za taasisi zilizo chini ya Tamisemi, Sh261.89 milioni ni maduhuli ya mikoa na Sh1.14 trilioni ni za mapato ya ndani ya halmashauri.”

 “Hadi Machi, mwaka huu, Sh863.78 bilioni zimekusanywa sawa na asilimia 72.02 ya lengo. Kati ya fedha hizo Sh848.14 bilioni ni mapato ya ndani ya mamlaka za Serikali za mitaa, Sh15.44 bilioni ni mapato ya ndani ya taasisi na Sh193.79 milioni ni maduhuli ya mikoa,” amesema.

Mchengerwa amesema makusanyo hayo yalitokana na ada za wanachuo, tozo, ukusanyaji wa madeni, mauzo ya bidhaa mbalimbali na ushuru unaotozwa na mamlaka za Serikali za mitaa kulingana na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290.

Amesema hali ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwenye mamlaka za Serikali za mitaa katika kipindi cha awamu ya sita imeendelea kuimarika; makadirio yameendelea kuongezeka kutoka Sh1.01 trilioni mwaka 2022/23 hadi Sh1.14 trilioni mwaka 2023/24.

“Makusanyo halisi yameongezeka kutoka Sh625.32 bilioni Machi, 2023 hadi Sh848.14 bilioni Machi, 2024 ikiwa ni ongezeko la Sh222.82 bilioni,” amesema.

Waziri amesema ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya ndani katika mamlaka za Serikali za mitaa, limechangiwa na mikakati inayofanywa na Tamisemi ikiwemo tathimini ya vyanzo vya mapato iliyofanyika kwa miaka miwili mfululizo ya mwaka 2022/23 na mwaka 2023/24 katika halmashauri 184, na matumizi ya mfumo wa Tausi katika ukusanyaji wa mapato.