Tamthilia ya Jua Kali yazoa tuzo tisa

Muktasari:

  • Tamthilia ya Jua Kali iliyosheheni mastaa mbalimbali imeshinda katika vipengele tisa katika tuzo za filamu.


Dar es Salaam.Tamthilia ya Jua Kali iliyosheheni mastaa mbalimbali imeshinda katika vipengele tisa katika tuzo za filamu.

 Tuzo hizo ambazo kwa mara ya kwanza zimesimamiwa na Serikali zimetolewa  jana Jumamosi  Desemba 18, 2021 jijini Mbeya ambapo vipengele 29 vilikuwa vikishindaniwa.

Pamoja na kuwepo kwa washindi mbalimbali, lakini tamthiliya ya Jua Kali imeonekana kutoa washindi katika vipengele vingi vilivyokuwa vikishindaniwa na kufika tisa.

Tamthiliya hii imemtoa msanii bora wa kike Godliver Gordian, ambaye amewabwaga washindani wake Christina Mroni, Tishi Abdallah na Johari Thabiti.

Pia imetoa mshindi katika kipengele cha mwongozaji bora wa kike ambaye ni Leah Mwendamseke akiwashinda Esie Esther, Christina Pande, Mariam Kaneji na Neema Ndepanya.

Vipengele vingine ilivyoshinda ni mwigizaji wa kiume msadizi, mwigizaji wa kike msaidizi, filamu yenye muziki mzuri, tamthilia bora na tamthilia  yenye muundo mzuri wa uzalishaji.