Tanesco kuokoa mabilioni iliyotumia kukodi vitendea kazi
Muktasari:
- Shirika limenunua bajaji 100, magari 100 na pikipiki 284 ambazo zimeanza kugawiwa katika ofisi za mikoa na wilaya za Tanesco kote nchini kwa ajili ya kuwafikia kiurahisi Watanzania.
Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kuokoa Sh1.3 bilioni kila mwezi, zilizokuwa zikitumika kukodi vitendea kazi vinavyotumika kwenda kuwahudumia Watanzania katika mwaka wa fedha 2024/25.
Kutokana na gharama hiyo, shirika limenunua bajaji 100, magari 100 na pikipiki 284 ambazo tayari zimeanza kugawiwa katika ofisi za mikoa na wilaya za Tanesco kote nchini kwa ajili ya kuwafikia kiurahisi Watanzania.
Vitendea kazi hivyo vimenunuliwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma katika maeneo mbalimbali hapa nchini, pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyakazi kote nchini katika kuwahudumia wateja.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowele leo Jumanne, Septemba 9, 2025, wakati wa mkutano na waandishi wa habari makao makuu Ubungo, Dar es Salaam.
Amesema vitendea kazi hivyo vitatumika katika madawati ya dharura kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja saa 24 kote nchini.
“Matokeo ya kununua vifaa hivi yanatokana na ziara ya Mkurugenzi wetu Mtendaji, Lazaro Twange, aliyoifanya mikoa mbalimbali nchini na kugundua kuna uhitaji mkubwa wa vitendea kazi hivi katika kuwahudumia wateja wetu kwa urahisi na wakati bila kujali maeneo waliyopo. Kama unafika kwa usafiri wa bajaji, magari au pikipiki, basi huduma itapatikana,” amebainisha.
Gowele ameongeza kwamba shirika limekuwa likitumia gharama kubwa kukodisha vifaa hivyo kutoa huduma, na katika mwaka wa fedha uliopita walitumia Sh1.3 bilioni kila mwezi.
“Hii itarahisisha kuwafikia wateja kwa wakati katika matatizo wanayokutana nayo. Vitendea kazi hivyo vinakwenda kuongeza nguvu, kwa sababu kwa sasa kuna magari yale ya dharura,” amesema.
Ametoa wito kwa watendaji wa Tanesco kuvitunza na kuvitumia kwa malengo, sambamba na kujali usalama wao wanapovitumia ili kuhakikisha wananchi wananufaika.
“Kulikuwa na adha kwa wafanyakazi ndani ya shirika, kwa kuwa vilivyokuwepo vilikuwa havitoshi, pia vilikuwa na gharama kubwa, hivyo ikaonekana uhitaji ili kunusuru hali hiyo,” amesema
Kwingineko, amesema hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme ipo kwa uhakika, ijapokuwa changamoto ndogondogo zinazojitokeza zinatokana na miundombinu.
Hata hivyo, amesema upande wa huduma kwa wateja malalamiko hayahusu kutopatikana kwa umeme, bali changamoto nyingine kama rimoti.
Katika hatua nyingine, Gowele amesema kazi ya ukaguzi wa mita za umeme za shirika hilo linaendelea nyumba kwa nyumba kote nchini, ambapo hadi sasa shirika limeendelea kuwabaini na kuwakamata wale wote waliokuwa wakichezea mita kwa lengo la kutolipa umeme.
“Nitoe wito kwa baadhi ya wateja wasio waaminifu kote nchini, waache mara moja kwani watafikiwa,” amesema.