Tanesco yatumia Sh611 milioni kutunza vyura Marekani

Muktasari:

  • Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imependekeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wizara za nishati pamoja na ya maliasili na utalii kuangalia namna ya kurejesha vyura wa Kihanzi waliopo nchini Marekani ili kupunguza gharama kwa Tanesco.

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetumia Sh611.92 milioni kutunza vyura wa Kihansi waliopo bustani ya wanyama nchini Marekani.

 Ripoti hiyo ya CAG ya mwaka 2021/22 imewasilishwa Alhamisi Aprili 6, 2023 bungeni jijini Dodoma ikielezea kiwango hicho cha fedha na mapendekezo aliyoyatoa kwa Tanesco, wizara ya nishati pamoja na wizara ya maliasili na utalii.

CAG Kichere amesema, mwaka 2000, Tanzania ilisafirisha vyura 500 kwenda bustani ya wanyama ya Bronx na Toledo iliyopo Marekani ili kuepuka hatari ya kupotea kwa vyura ambayo ilitokana na utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji wa Kihansi mwaka 1994.

“Ingawa haiwezekani kubainisha idadi kamili ya sasa ya vyura vinavyosimamiwa nchini Marekani, Tanesco linagharamia dola za Marekani 130,000 kwa mwaka kwa ajili ya kutunza vyura hao, ambapo inakadiriwa takribani ya dola za Marekani milioni 2.86 zilitumika kwa miaka yote 22 ya kuhudumia vyura,” anasema CAG Kichere na kuongeza:

“Katika mwaka 2020/21 na 2021/22, ilifanya malipo ya Sh611.92 milioni (sawa na dola za Marekani 260,000).

“Nimebaini kuwa mkataba kati ya Tanzania na bustani za wanyama za Marekani ulimalizika mnamo Juni 2020 na kuongezewa muda wa miaka miwili hadi Juni 2022.”

CAG KIchere amesema, japokuwa hakukuwa na mpango wowote wa kurudisha vyura hao Tanzania ikizingatiwa tayari miaka 22 imepita tangu vyura 500 wapelekwe kwenye bustani za wanyama za huko Marekani, “ninapendekeza Shirika la Umeme Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Wizara ya Maliasili na Utalii iweke mpango mkakati wa kurudisha vyura wa Kihansi ili kuepuka gharama kwa Shirika la Umeme Tanzania.”