Miaka 18 ya uhifadhi vyura wa Kihansi

Chura wa Kihansi ambao kitaalamu hufahamika kama ‘Nectophrynoides asperginis’

Muktasari:

  • Hawa ni vyura wenye sifa za kipekee, ikiwamo kubwa ya kuwa aina ya vyura wanaopatikana Tanzania pekee

Unafahamika kama Mto Kihansi ambao unafanya maporomoko katika milima ya Udzungwa unaoanzia Mufindi na Kilolo mkoani Iringa. Mto huu humwaga maji yake katika Bonde la Kilombero, Morogoro.

Eneo hilo la milima lina sifa nyingi za uhifadhi, lakini kupatikana kwa vyura aina ya nectophrynoides asperginis mwaka 1996 ambao walipachikwa jina la vyura wa Kihansi, kumelifanya liwe la kipekee ulimwenguni.

Upekee huo unapambwa na ukweli kuwa vyura hao ni kati ya viumbe ambao wanapatikana Tanzania pekee na wapo katika orodha ya viumbehai walio katika hatari ya kutoweka.

Kutokana na hali hiyo Vyura wa Kihansi wapo katika orodha ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanyama na Mimea iliyo Hatarini Kutoweka (Cites), hivyo hivi sasa wanalindwa kisheria na ni mafuruku kuwauza  sehemu yoyote duniani.

Sifa za kipekee

Awali haikufahamika vyura hao kuwapo katika eneo hilo mpaka mradi wa uzalishaji wa megawati 180 za umeme ulipoanza kutekelezwa katika bonde hilo mwaka 2006.

Viumbehai hao, wanaishi kwenye mazingira ya maji yanayotiririka na kutoa mvuke mwingi unaosababishwa  na nguvu ya maji. Sifa yake kuu ni kutaga mayai na kukaa nayo kwenye kifuko kilichopo ndani yake hadi muda wa kuanguliwa unapofika.

Wakati ukifika vyura hao hutoa vitoto hai hali ambayo kisayansi hutafsiriwa kuwa ni kuzaa. Kutokana na ukweli kuwa hatagi mayai yakaonekana,  ni dhahiri kuwa vyura wa jamii ni tofauti na jamii nyingine duniani ambao hutaga mayai yanayoonekana.

Vyura wa kawaida hutaga mayai na kuyaacha majini yakielea katika utando na kisha huanguliwa wakati unapowadia, lakini wa Kihansi huangulia tumboni.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake zimeandaa mradi wa awamu ya pili wa miaka mitano ya utunzaji wa mazingira katika Bonde la Mto Kihansi  ambao unasimamiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC).

Wadau wengine ni Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri), Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), Benki ya Dunia (WB) na mashirika wahisani lengo likiwa kurudisha uoto wa asili uliokuwepo ili kuwafanya vyura hao waishi katika eneo lao hilo la asili.

Kulingana na vyanzo mballimbali, vyura wa Kihansi alitangazwa rasmi kuwa ametoweka katika mazingira yao ya asili Novemba  2009 na chanzo kikuu kikitajwa kuwa ni ujenzi wa bwawa la umeme la Kihansi mwaka 1999/2000.

Matumizi ya maji

Bwawa hilo linaelezwa kutumia karibu asilimia 90% za maji yaliyokuwa yanapita ndani ya makazi ya vyura na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa uhifadhi wa mazingira kama Wildlife Conservation Society na Benki ya Dunia ikafadhili mradi wa awali kuwanusuru vyura wa jamii hiyo.

Katika utekelezaji wa mpango huo, vyura wapatao 500 walipelekwa katika Chuo Kikuu cha Colorado nchini Marekani na jitihada zikifanyika kufufua makazi yake ya asili ambayo yaliathiriwa na utekelezaji wa mradi huo wa umeme. Mtafiti na mhitimu wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Hawaii cha  Mareka, Devolent Mtui  anasema mfumo bandia ulizalisha vyura zaidi ya 20,000 kutoka 1,200 waliokuwepo mwaka 2003.

Mtui ambaye alifanya kazi katika mradi wa awamu ya kwanza wa Usimamizi wa Maendeleo ya Maporomoko ya Kihansi ambao ulikoma 2011, anabainisha kuwa mwaka 2009 vyura hao ghafla walitoweka. Anasema taarifa za wataalamu zinataja sababu za kutoweka kwao kuwa huenda zinasababishwa na aina fulani ya fungus, waitwao chytrid au kemikali zinazotokana na mbolea zinazotumiwa na wakulima kwenye vyanzo vya maji yanayotiririka katika mto huo.

Anaongeza kuwa vyura waliopelekwa Marekani wameendelea kuzaana na kwa mujibu wa mkurugenzi wa mipango na utafiti wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Fadhila Khatibu hadi sasa vyura 3,000 wamerudishwa.

Khatibu anasema baadhi ya vyura hao wamehifadhiwa Chuo Kikuu Dar es Salaam na wengine walirudishwa kwa awamu wapo katika makazi yao ya asili.

Anaongeza kuwa awamu ya pili ya mradi huo wa miaka mitano kuanzia sasa hadi Desemba 2018, utagharimu kiasi cha Sh5.98 bilioni na umelenga kukabiliana na changamoto za awali ambazo ni pamoja na elimu kwa wakazi wanaozunguka mradi.

Anasema:  “Wakazi wa vijiji 30 vilivyopo katika wilaya tatu zinazozunguka mradi huo ambazo ni Mufindi, Kilolo na Kilombero  wataelimishwa umuhimu wa kutunza mazingira ili kuwanusuru viumbe hao.”

Anasema  elimu itahusu kupunguza matumizi ya maji kwa ajili ya shughuli za kilimo, kuzuia ukataji miti, utunzaji na uhifadhi wa mazingira ya eneo hilo na kuhakikisha maji hayo hayachafuliwi kwa shughuli za binadamu.

“Tunataka kupunguza matumizi ya maji kwa ajili ya shughuli za kilimo kwani mbolea na takataka nyingine zina athari kwa vyura hao na viumbe wengine wanaotegemea mto huo,” anasema na kuongeza kuwa kutakuwa na mashamba darasa pia.

Anasema mashamba hayo, ambayo yatasimamiwa na wataalamu wa masuala ya kilimo, yatatumika kuwafundisha wakulima wa maeneo hayo namna nzuri ya ulimaji ambayo haichafui uoto wa asili wa eneo hilo.

Meneja mwandamizi wa utafiti na mazingira wa Shirika la Umeme (Tanesco), Aaron Nanyaro anasema ingawa shirika lake linachohitaji ni kufua umeme kwa ajili ya shughuli za maendeleo, linatambua kuwepo kwa viumbe hao na kwamba linasaidia katika utunzaji wa mazingira.

Anasema kutokana na hali hiyo, shirika lake limepunguza mita za ujazo 1.5 ambazo zingeweza kuzalisha kiasi cha megawati 7 za umeme, ili kiasi hicho cha maji kiende kwa vyura hao, pia kuna mashine za kisasa za kutawanya maji hadi katika makazi ya vyura hao.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Utafiti wa Wanyamapori (Tafiri), Simon Mduma anasema anasema Serikali imeingia mikataba mingi ya kimataifa ya uhifadhi na kuhakikisha uwepo wa viumbe walio hatarini kutoweka, lakini mafungu kwa ajili ya utafiti ni tatizo.

Anasema awali walipewa jukumu la utafiti wa kuwepo kwa vyura hao, kuwezesha wawepo, uhifadhi wa Kihansi, kiwango cha maji, utafiti wa viumbe wengine wanaopatikana Kihansi na utafiti wa upunguzaji wa kiasi cha dawa zinazotumika shambani.

Mduma anasema hata hivyo kiasi cha Sh. 250 Milioni walizoomba kwa kazi hiyo toka Serikalini,  walipata pungufu hali ambayo iliwafanya wajikite katika eneo moja la kuwezesha kuwepo kwa vyura hao pekee.

Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (Nemc), Boniventure Baya anasema kuzinduliwa kwa mpango wa awamu ya pili wa miaka mitano wa uhifadhi wa bonde hilo, umelenga kuwahakikishia vyura wapatao 5,000, wanapata sehemu salama ya kuishi.

Anasema uhai wa vyura hao unategemea ushirikiano na wadau ambao watafikiwa na mradi huo wakiwemo wakulima ambao matumizi yao ya maji na viwango vya viuatilifu wanavyotumia, ndivyo vitu vya msingi ambayo vitawanusuru vyura hao.