Tanroads Kigoma yatoa maelezo mipasuko mikubwa kwenye barabara

Muktasari:

  •  Kipande cha barabara chenye urefu wa mita 50 kimepata mipasuko mikubwa eneo la Busunzu, wilayani Kibondo, mkoani Kigoma.

Kigoma. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Kigoma umetoa ufafanuzi kuhusu mipasuko kwenye barabara eneo la Busunzu, wilayani Kibondo.

Ufafanuzi huo unatokana na picha jongefu (video) iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii jana Machi 26, 2024 ikionyesha mipasuko mikubwa kwenye kipande cha barabara cha urefu wa mita 50 eneo la Busunzu, barabara kuu ya Kigoma kwenda Mwanza.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma kupitia video ameeleza eneo hilo ni la mradi unaotekelezwa na mkandarasi kutoka China anajenga barabara yenye urefu wa kilomita 59.35 kwa kiwango cha lami.

Choma amesema Tanroads tangu Februari 24, 2024 walipewa taarifa na mkandarasi mshauri, Kampuni ya Sila kutoka nchini Mali ikishirikiana na Kampuni ya Kitanzania ya Nibu, kwamba wameanza kuona mipasuko katika eneo hilo la barabara.

“Tuliwashauri waendelee kuiangalia lakini baada ya siku mbili waliona kama mipasuko inaongezeka kila kukicha. Wakashauri tuendelee kuangalia hali inaendaje lakini sisi Tanroads tulichukua hatua ya kukihusisha kitengo chetu cha uchunguzi wa kimaabara na vifaa (RDO), ili kufanya uchunguzi wa kina kwa sababu wana vifaa vya kisasa,” amesema Choma.

Picha ikionyesha eneo la barabara lililopasuka.

Amesema walifanya uchunguzi wa haraka na kubaini eneo hilo kuna tatizo la mabadiliko ya kimazingira ambalo lilihitaji uchunguzi wa kina na kwa sasa wanaendelea.

Choma amesema kwa kuwa barabara hiyo ilishaanza kutumika walimwelekeza mkandarasi mshauri afunge eneo hilo lisiendelee kutumika kwa sababu linaweza kuwa hatari kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Amesema kwa sasa magari yanapita pembeni ya barabara, akieleza ni matumaini yake kuwa uchunguzi utakapokamilika watajua tatizo ni nini na hapo ndipo watajua watafanya nini.

Amesema kama itaonekana ni tatizo la kimazingira basi watashauriwa hatua gani za  kuchukua ili kuondoa tatizo lisiweze kutokea tena.

“Tumeamua kufungua macho katika maeneo mengine, hatutaishia eneo hili tu. Tutaangalia na maeneo mengine yenye matatizo hayo. Wanaofanya uchunguzi watapitia na maeneo mengine yote ili kuepuka shida kama hii isijitokeze tena,” amesema Choma.

Amesema usanifu wa barabara hiyo ulifanyika na kuonyesha eneo hilo la mlima lazima likatwe kuupunguza uliokuwepo na ilifanyika hivyo.

Baada ya mlima kukatwa amesema walipima uwezo wa udongo huo na kuendelea kuweka tabaka lingine juu.

Amesema iwapo uchunguzi utabaini makosa ya mkandarasi au kiutendaji basi hatua stahiki zitachukuliwa.

Kutokana na hilo, amewataka wananchi wa Mkoa wa Kigoma wasiwe na wasiwasi, kwani wataendelee kufuatilia kwa karibu kujua tatizo ni nini ili waweze kupata barabara bora na yenye viwango.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema mkandarasi atumie tatizo hilo kama faida kwakwe ili tatizo kama hilo lisiweze kujitokeza tena katika eneo lingine.

Ujenzi bado unaendelea lakini eneo hilo linahitaji uangalifu zaidi kwa sababu ya mabadiliko ambayo yanaendelea kwenye jiografia.

Amesema pengine eneo hilo linahitaji uangalizi na utaalamu mkubwa zaidi wa kufanya barabara hiyo isipate tena tatizo kama hilo.

“Nitoe wito kwa wakandarasi muda huu ambao bado wanaendelea na ujenzi kurekebisha maeneo ambayo wameona kuwa na upungufu, lakini naamini wao pia wameyaona zaidi hata tuliyoona sisi ili kuhakikisha tunapata barabara bora kama ilivyoahidiwa,” amesema Andengenye.