Tanroads wakanusha kuharibika kwa uwanja wa ndege Chato

Meneja wa wakala wa barabara mkoani Geita (aliyevaa koti) akiwa na mkuu wa kitengo cha miradi Robert Shilangale wakikagua njia ya ndege (run way) iliyodaiwa kuwa na mpasuko na nyasi.
Muktasari:
- Tanroads Geita yakanusha uvumi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii za kuharibika kwauwanja wa ndege wa mkoa wa Geita.
Chato. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Geita imekanusha taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha uwanja wa ndege wa Geita ukiwa na mipasuko na nyasi, ikisema ni za uzushi na zenye lengo la kuhujumu uwanja huo.
Akizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi wa njia za ndege, Meneja wa Tanroads mkoani hapa, Haruna Senkuku amesema uwanja huo upo kwenye hali ya ubora na ndege zinatua mara tatu kwa wiki.
“Ndege ziko kwenye viwango vya juu vya ubora na umehakikiwa na mashirika yote yanayohusika na viwanja vya ndege uwanja huu unatumiwa na ndege za ndani na nje kama mtakumbuka wamewahi kutua marais kutoka Kenya, Uganda na Msumbiji na wikiijayo tunategemea kupewa leseni ya moja kwa moja ya uwanja,” amesema Senkuku.
Ofisa usalama uwanja huo, Hellen Osoro amesema uwanja huo hutumika kila siku za jumatatu, Alhamisi na jumamosi kwa ndege za abiria za shirika la ndege la ATCL.
Uwanja wa ndege Geita ulijengwa na mkandarasi wa ndani ambae ni Mayanga Constraction chini ya usimamizi wa wakala wa barabara mkoani hapa kwa gharama ya Sh 58 bilioni ambazo ni fedha za ndani.