Tanroads, Tarura Tanga waombwa kuweka matuta yenye ubora

Muktasari:

  •  Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Tanga, wameilalamikia Taasisi ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kwa uwekaji wa matuta makubwa yanayosababisha uharibifu wa vyombo vya moto na kuwa kero kwa watumiaji wa barabara mkoani humo.


Tanga. Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Tanga, wameilalamikia Taasisi ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kwa uwekaji wa matuta makubwa yanayosababisha uharibifu wa vyombo vya moto na kuwa kero kwa watumiaji wa barabara mkoani humo.

Wakichangia hoja katika kikao hicho wajumbe hao wamesema taasisi hizo zizingatie ubora na umuhimu wa eneo husika katika uwekaji wa matuta maarufu rasta ambayo wamesema yamekuwa hayana msaada kwa mtumiaji na badala yake yanasababisha uharibifu.

Akichangia hoja hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Sirieli Mchembe amesema uwekaji wa matuta uzingatie sheria hasa maeneo ya barabara kuu ili kuondoa changamoto ya kero kwa watumiaji wa barabara kubwa.

"Matuta hatukatai lakini yafuate sheria za matumizi ya barabara kuu maana eneo unalotakiwa kwenda spidi 80 unatembea 20, hii si sawa wenzetu Tanroads muiangalie hii kero, tuige mifano ya nchi za wenzetu za Afrika Mashariki," amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashimu Mgandilwa amezungumzia ubora wa matuta madogo maarufu rasta katika barabara za mitaani ambapo amesema matuta hayo yamekuwa kero na kwamba yanasababisha baadhi ya barabara za mitaa kutopitika kwa kukwepa matuta hayo.

Akijibu malalamiko hayo Meneja wa Tarura Mkoa wa Tanga, Mhandisi George Tarimo amesema amepokea malalamiko ya wajumbe wa kikao hicho na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kurekebisha matuta hayo.