Tanroads yaanza kurekebisha kona kali barabara ya Kitonga

Moja ya eneo ambalo barabara ya Mlima Kitonga mkoani Iringa inapanuliwa

Muktasari:

  • Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Iringa imeanza kupanua barabara hasa kwenye kona kali baada ya kuwepo malalamiko ya foleni na ajali.

Iringa. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wameanza kupanua barabara ya Mlima Kitonga hasa kwenye maeneo ya kona kali, ili kupunguza foleni na ajali za mara kwa mara kwenye eneo hilo.

 Akitoa taarifa kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa waliotembelea barabara hiyo jana Janauri 31, 2024 Meneja wa Tanroads Mkoa wa Iringa, Yudas Msangi amesema zaidi ya Sh6.4 bilioni zitatumika kwenye upanuzi huo.

Hivi karibuni, baadhi ya wakazi wa eneo hilo, madereva na abiria wanaotumia barabara hiyo wamekuwa wakilalamika kuwepo kwa foleni hasa inapotolea ajali na kuziba barabara.

Msangi amesema kutokana na hali hiyo, wameamua kutafuta suluhisho la muda mfupi na mrefu, ili kutatua changamoto kwenye mlima huo.

"Suluhisho la haraka ilikuwa ni kupanua barabara maeneo yenye kona kali, ili kupunguza msonganano kazi ambayo inaendelea kufanyika," amesema.

Mafundi wakiendelea kupasua miamba katika barabara ya Kitonga ambayo inapanuliwa

Kuhusu suluhisho la muda mrefu, Msangi amesema linaendelea kufanyiwa kazi kwa mkandarasi kuendelea na uchunguzi, ili kujua njia ipi rahisi itasaidia kutatua kero za usafiri kwenye mlima huo.

"Mkandarasi yupo kazini na atatuletea majibu au tuwe na njia ya mchepuo au njia nne," amesema Msangi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amesema kazi na matengenezo ya barabara kwenye mlima huo zitafanyika kwa umakini, ili magari yaendelee kupita.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yassin amesema upanuzi wa barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa nchi.

"Bajeti ya upanuzi wa barabara hii haukuwepo, lakini kwa umuhimu wake Serikali imetoa fedha," amesema Yassin.

Baadhi ya madereva wa magari makubwa wameiomba Serikali ya Mkoa wa Iringa kuwa na gari la kuondoa magari yanayopata ajali, ili kupunguza foleni linapotokea tatizo hilo.

"Ikitokea ajali tunakaa hapa hadi saa sita kusubiri liondolewe, maeneo kama haya muhimu kukawa na gari hata moja la kusaidia kutoa magari yaliyoangukia na kuziba njia," amesema Elia Dandi, dereva wa lori.