Tanzania,China zakubaliana kuimarisha ushirikiano

Muktasari:

Pande zote mbili zimekubaliana kuendelea na kuimarisha ushirikiano  utakaowezesha kupatikana kwa fedha kwenye uwekezaji wa miundo mbinu ya kilimo na viwanda vidogo vidogo vya uongezaji thamani kwenye mazao ya kilimo kwa wakulima nchini.

Dar es Salaam.Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imefanya mazungumzo na Taasisi muhimu za kifedha na kiuchumi nchini China kwa ajili ya upatikanaji wa fedha za uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu na viwanda nchini .

Ujumbe wa TADB umeoongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ,  Francis Assenga alipokutana na Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya China (CBD) leo  kwenye Mkutano uliofanyika, Guangzhou, China.

Pande zote mbili zimekubaliana kuendelea na kuimarisha ushirikiano  utakaowezesha kupatikana kwa fedha kwenye uwekezaji wa miundo mbinu ya kilimo na viwanda vidogo vidogo vya uongezaji thamani kwenye mazao ya kilimo kwa wakulima nchini.
Katika ziara hiyo TADB pia imefanya majadiliano ya kina na Mfuko wa Maendeleo ya Africa wa China (China African Development Fund) ambao hufanya uwekezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo na ya kibiashara (Equity investmenta) kwenye nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Ujumbe wa ulioongozwa na Makamu Mtendaji wa Rais na Naibu Mtendaji Mkuu wa 'CADFUND' . Wang Yong aliyefuatana na Mkurugenzi Mkuu wa Sekta ya Viwanda, Kilimo, Afya na Uwekezaji, . Lei Ma; Mkurugenzi Mkuu wa Maendeleo ya Masoko na Huduma Elekezi , Henry Liu na Meneja wa Uwekezaji wa Viwanda, Ardhi na Kilimo  Luo Zhongquan.

Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu wa Viwanda Biashara na Uwekezaji (UWEKEZAJI), Prof. Adolf Mkenda. Wengine waliohudhuria ni Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki; na Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini China Lusekelo Gwassa.
Katika mazungumzo hayo, pamoja na mambo mengine CADFUND walikubali kuendelea kutoa fedha kwenye miradi ya kiuchumi na uwekezaji mkubwa kwenye nyanja za  kilimo, madini na miundombinu kama ya maji na umwagiliaji.