Tanzania ilimwita waziri mstaafu, Rondo mfalme

Safari inaanza kutoka Dar es Salaam, jiji lenye kila tafsiri ya Utanzania. Unafuata uelekeo wa Mbagala unaivuka hadi Kongowe. Miji inabadilika kutoka Kimanzichana hadi Kibiti. Ramani ya Google inautafsiri mwendo kuwa tunakatiza kando ya Bahari ya Hindi.

Vipimo vinaonesha kuwa kutoka Dar es Salaam hadi Lindi ni umbali wa kilomita 460 kama unasafiri kwa gari, na kilomita 356 ikiwa unapaa kwa ndege. Ni safari ya hisia. Kwenda kumpumzisha mmoja wa watoto halisi wa Tanzania, aliyeyatoa maisha yake kuutumikia umma.

Bernard Kamillius Membe, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70 kasoro miezi sita. Miaka zaidi ya 40 aliyoutumikia umma wa Watanzania kabla ya kustaafu, kikokotoo chake kinaonesha kuwa takriban asilimia 64 ya maisha aliyatumia kuihudumia Jamhuri ya Muungano.

Bahati mbaya, hakuna tathmini ambayo inaweza kutoka ili kujenga makisio japo ya kifikra ni kiasi gani Tanzania leo ina unafuu mkubwa kwa sababu ya utumishi wa Membe.

Shairi la “Character of the Happy Warrior” – “Uhusika wa Shujaa Mwenye Furaha", lililoandikwa na mwandishi William Wordsworth, Septemba 3, 1802, linaweza kutusaidia kuielewa thamani ya Membe.

Wordsworth aliandika kuwa shujaa mwenye furaha ni yule ambaye kila askari angependa kuwa kama yeye.

Katika shairi hilo, mistari ya mwishoni, Wordsworth aliandika kuwa shujaa mwenye furaha lazima aizunguke dunia kufanikisha malengo. Na hata kama atakufa pasipo matokeo aliyokusudia, atakuwa mwenye furaha kipindi pumzi yake inakata, huku akipigiwa makofi mbinguni. Membe tangu uvulana wake alitamani kuutumikia umma. Kufanikisha viwango vya kutimiza malengo, alisoma Rondo-Chiponda kisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Haitoshi, alifika hadi Chuo Kikuu cha John Hopkins, Washington DC, Marekani.

Ni mseminari. Ndipo bila shaka alijengwa kimaadili. Baada ya kutoka Rondo-Chiponda na kabla ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Membe alipita Seminari za Namupa, Lindi na Itaga, Tabora.

Akiwa kijana wa miaka 24, tayari alikuwa Ofisi ya Rais, akiwa mchambuzi wa masuala ya usalama wa taifa.

Alipokuwa na miaka 35, taifa lilimtuma Canada, akawa msaidizi wa Balozi wa Tanzania. Alipofikisha umri wa miaka 46, aliona ni wakati sahihi kuwahudumia wananchi wa jimbo lake.

Aliingia kwenye siasa, aligombea ubunge jimbo la Mtama, Lindi, akashinda na kuhudumu kwa miaka 15.
Alipokuwa bungeni, kwa nyakati tofauti, taifa kupitia Rais, lilimpa Membe majukumu ya Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani, kisha Nishati na Madini, baadaye akafika utumishi wa juu kabisa katika safari yake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Baada ya tangazo la kifo cha Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, alisema: “Membe alikuwa mtu aliyetosheka. Mara nyingi alipenda kukaa kijijini kwake na kushirikiana na wanakijiji.”

Kwa mujibu wa Mkuchika, mara kwa mara alikuwa akikutana na Membe. Siku zote mwanausalama na mwanadiplomasia huyo aliyebobea, alionesha kuridhika na kila hatua aliyopiga kwenye maisha yake ya utumishi na mavuno aliyopata.

Kwamba hakuwa tajiri ila alitosheka. Na kwa kurejea maneno ya Wordsworth, bila shaka Membe alitabasamu kwa furaha, huku akipigiwa makofi mbinguni.

Maana alitosheka na kusudi lililomleta duniani.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tehama, Nape Nnauye, alitoa ushuhuda wake kuwa mwaka 2010, Membe alimwita akagombee ubunge Mtama. Kwa kifupi, Membe alikuwa tayari kumwachia Nape jimbo tangu mwaka 2010.
Kwa mujibu wa Nape, alikataa ‘ofa' hiyo ya Membe, akachagua kugombea ubunge jimbo la Ubungo, lakini alishindwa kwenye kura za maoni CCM. Kisha, Membe alimwita, akamwambia:

“Kugombea Ubungo haukuwa uamuzi sahihi. Mwaka 2015 uje Mtama, sitagombea.”

Kweli, mwaka 2015, Membe hakugombea, badala yake alimshika mkono Nape, mtaa kwa mataa kuhakikisha anashinda. Nape alishinda ubunge Mtama, na anaendelea muhula wa pili.

Ni uthibitisho kuwa Membe alitosheka. Baada ya vipindi viwili vya ubunge, alitaka kuacha jimbo, kilipotimia cha tatu, alistaafu ubunge. Kisha alibaki kuwa mtu mwenye furaha. Nape na Mkuchika wanathibitisha hilo.

Ujumbe unaoupata hapo ni kuwa Membe aliyakadiria maisha yake vema. Ndio maana hakung'ang'ana na ubunge wala vyeo vya uteuzi serikalini. Baada ya uwaziri, alibaki raia mwenye furaha.

Kwa vile aliyakadiria maisha yake vema, Membe hakuona tabu kuuonesha upande wake wa pili wa kibinadamu, kipindi cha uongozi wa Rais John Magufuli; uanaharakati! Membe alisimama kama mwanaharakati asiyeogopa kumpa changamoto Magufuli ndani ya CCM, alipoona mambo hayapo sawa. Hata alipofukuzwa CCM, alihamia ACT-Wazalendo, akagombea urais.

Shabaha kuu ya Membe ilikuwa kumpinga Magufuli tena kwa uwazi, na alisimama hivyo mpaka mwisho. Membe alirejea CCM baada ya hatamu kushikwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Turejee safari ya msibani

Ukishafika Lindi, unahesabu kilomita 55 kufika Rondo. Hicho ndicho kijiji alichozaliwa Membe, alianzia masomo hapo, na pamekuwa nyumbani kwake siku zote za maisha yake. Angezunguka dunia yote, ila mwisho angerejea Rondo.

Angeishi Dar es Salaam na kufanya shughuli zake za siku baada ya siku, lakini maskani kuu ya maisha yake yalikuwa Rondo. Mwisho kabisa, tandiko la usingizi wake wa mwisho limekuwa Rondo.

Ukiwa Lindi unauona msiba wa Membe kwenye macho ya watu. Safari inaendelea hadi kijiji cha Ngongo. Ni umbali wa kilomita 16 kutoka Lindi Mjini. Nyuso za watu zinakiri msiba ni mkubwa kwao.

Kutoka Ngongo hadi Rondo, zinatimia kilomita 39. Hapa ndipo maskani kuu ya Membe. Wazazi wake waliishi hapo, naye akaendeleza urithi. Rondo, unakutana na watu ambao nyoyo zao zimepondeka. Bado hawaamini kama kweli Membe ameondoka. Walimwamini na kumtumaini mno na kwao alikuwa shujaa.
 

Wananchi bado hawaoni na hawadhani kama yupo mwingine kama Membe. Huyu ni alama kwenye maisha yao. Shule ya Rondo-Chiponda, ambayo alisoma, majengo yake yalikuwa ya tope.

Membe aliibomoa na kuijenga upya kwa saruji, sasa imekuwa ya kisasa kwelikweli.

Membe alijenga madarasa ya awali kwenye shule hiyo ili watoto wa Rondo na Chiponda waanze kusoma kuanzia chekechea. Wao hawajui ushiriki wa Serikali, daima humwona Membe na juhudi zake binafsi.
Rondo ina soko kubwa la kisasa.

Wananchi wa Rondo wanasema lilijengwa na Membe kwa juhudi binafsi, kisha akalikabidhi kwa halmashauri, ili waliendeshe. Ni soko la kiwango cha masoko ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa wana-Rondo, soko hilo, sio tu kwamba limejengwa na Membe, bali pia hata kiwanja ambacho kimetumika ni chake. Vyote hivyo alivitoa kwa jamii kwa maendeleo ya Rondo.

Zahanati ya Rondo, wanakijiji wanaita hospitali. Huwaambii kitu tofauti kuwa Serikali ndio ilijenga. Wao wanatoa ushuhuda kwa kujiamini kuwa hospitali yao imejengwa kwa juhudi binafsi za Membe, na hata kiwanja kilichotumika ni mali yake pia.

Rondo kuna msikiti mzuri wa kisasa, ambako waumini wanasali, kisha wanamwombea dua Membe. Msikiti huo ulijengwa na Membe mwenyewe.

Majonzi yapo wazi, kwani, mchango wa Membe kwao hauna kifani.
Sio tu kwa kujenga msikiti, bali ushuhuda unatolewa kuwa kila mwaka, Membe aliwezesha waislamu saba hadi nane kwenda kuhiji Makka. Nani mwingine wa kuziba pengo hilo? Ukiwa msikitini unakutana na mahujaji wa Makka wa miaka tofauti, waliofanikishiwa ibada zao za hija na Membe. Ameacha maumivu sana.

Membe alikuwa Mkristo, tena Mkatoliki, ila hakuwa mdini. Ndio sababu hakuwa na hiana kusaidia ujenzi wa msikiti. Hata alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, alitetea waziwazi Tanzania kujiunga na Chama cha Ushirikiano wa Kiislam (OIC).

Mei 15, 2023, mwili wa Membe uliwasili Rondo. Ratiba ilionesha misa kwa siku hiyo ingefanyika nyumbani kwake. Hata hivyo, Kanisa Katoliki Usharika wa Rondo, uliomba ibada hiyo ifanyikie kanisani kwao, ili kwao iwe misa ya shukurani kwa Membe.

Kwa nini? Membe ndiye alijenga kanisa hilo. Uongozi wa kanisa ukaona hautamtendea haki kama halitaendesha misa maalumu ya shukurani kwake. Kifo cha Membe kimegusa madhabahu kanisani hadi mihrab msikitini.

Akina mama na vijana, wanalia kwa namna tofauti. Wapo wanaoguswa kwa jinsi Membe alivyobadili maisha yao, na sasa kawaacha, wengine ni waliokuwa na matarajio chanya kupitia maisha yake lakini amekatika.

Kila mwaka, Membe alikuwa na utaratibu wa kusaidia mitaji ya biashara kwa vikundi vya akina mama na vijana. Hakutaka kumsaidia mmojammoja, aliamini katika vikundi, ili pia wanapojiendeleza inakuwa rahisi kukopesheka.

Membe alidhamini vikundi vingi vya Rondo kupata mikopo benki ili kukuza mitaji yao ya kibiashara na kuzidi kujikwamua kimaisha. Kitendo hiki kilisaidia mno mzunguko wa kifedha Rondo na ukuaji wa kiuchumi. Wananchi wanawaza bila Membe itakuwaje. Na kwa hakika, Membe ameondoka akiwa ni Shujaa Mwenye Furaha.