Tanzania inavyopiga hatua kufikisha mawasiliano vijijini

Muktasari:
- Serikali imeendelea kutilia mkazo huduma ya mawasiliano vijijini baada ya kuendelea kujenga minara mipya.
Kigoma. Serikali imeendelea na ujenzi wa minara mipya ya mawasiliano kurahisisha huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza hayo leo Julai 17, 2024 Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alipofika katika mikoa ya Kigoma na Geita katika ziara maalumu, ikiwa ni mpango wake wenye lengo la kukagua na kujionea utekelezaji wa ujenzi wa minara mipya ya mawasiliano inayojengwa na wadau wa mawasiliano katika mikoa mbalimbali chini ya usimamizi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote UCSAF kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
Nape amekagua mnara mpya wenye teknolojia ya 4G uliojengwa na Airtel Tanzania Kijiji cha Kumbanga mkoani Kigoma na kuendelea na ziara yake ambapo wiki hii anatarajia kukagua minara mingine miwili iliyojengwa na Airtel mkoani Geita kijiji cha Nyakagomba na Busonzo. Katika ziara hiyo, Waziri ameipongeza Airtel Tanzania kwa jitihada zake za kushirikiana na Serikali katika kuinua na kusambaza mawasiliano ili kuziba mgawanyiko wa kidijitali katika jamii za vijijini ambazo hazijafikiwa na mawasiliano.
Minara hiyo mitatu ni sehemu ya mpango wa Airtel Tanzania unaofadhiliwa na UCSAF na Benki ya Dunia chini ya mradi wa DTP ambapo ujenzi wake unalenga kuwezesha na kuboresha mawasiliano katika maeneo ambayo hayajawawahi kufikiwa na huduma yeyote ya mawasiliano.
Airtel Tanzania, katika mpango huu wa kusambaza mawasiliano vijijini tayari imekamilisha ujenzi na kuwasha minara 84 ya 4G, ikijumuisha minara hii ya Kigoma -Kumbanga, Geita-Nyakagomba na Busonzo.
Nape, amesema kuwa Serikali iliweka ruzuku ya shilingi milioni 100 na kwa kushirikiana na mtandao huo mnara huo utaleta faida.
“Huduma nyingi za Serikali zinaenda mtandaoni na unaweza ukazipata ukiwa hapa hapa kijijini kwa kutumia huduma hizi za mawasiliano. Huu mnara ndio benki yenu. Mnaweza mkalipana, mkanunua, mkafanya mambo yote kupitia mnara huu,” amesema Nape
Minara hii mitatu ya mtandao huo inatarajia kubadilisha maisha ya wananchi wa maeneo haya kwani itawawezesha kupata huduma mbalimbali za kidijitali kupitia simu za mkononi ambazo sekta zao zimeunganishwa ili kutoa huduma kama vile elimu, afya na kilimo.
Kwa upande wake, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, ameeleza kuwa uwepo wa mnara huo umeleta unafuu kwenye mawasiliano ya simu kinyume na ugumu uliokuwepo hapo awali.
“Mawasiliano yalikuwa ya shida sana. Mpaka upande kwenye kichuguu ndo upate kuwasiliana lakini baada ya kutuletea huu mnara sasa hivi tunawasiliana vizuri na maendeleo yanaenda vizuri,” amesema
Naye, Meneja Mauzo wa Kanda ya Airtel, Isack Kijuu alieleza kuwa uanzishaji wa minara hiyo mitatu unadhihirisha dhamira ya Airtel Tanzania katika kuinua na kuleta mabadiliko chanya maeneo ya vijijini kupitia teknolojia ya hali ya juu.
“Lengo letu la pamoja na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari ni kuboresha maisha ya Watanzania kupitia mpango huu wa Tanzania ya Kidijitali, tunahakikisha kwamba ushirikishwaji wa jamii katika kupata huduma za kidijitali si dhana ya kufirika tena. Ni jambo muhimu na wanastahili kupata mawasiliano ya uhakika," Ki VPjuu ameeleza