Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania katika mtihani mwingine jumuiya ya kimataifa

Muktasari:

  • Jumuiya ya Madola imeitaka Tanzania ndani ya siku 90 kufanya mambo saba, yakiwemo mageuzi ya mifumo yake ya uchaguzi.



Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeingia katika mtihani mwingine ndani ya jumuiya ya kimataifa, baada ya Jumuiya ya Madola kuitaka iondoe zuio la uhuru wa kukusanyika na kujieleza, huku ikitoa miezi mitatu ya kufanyika mageuzi ya mifumo ya uchaguzi na ushindani wa kisiasa.

Maelekezo hayo ya jumuiya ya madola, yametolewa baada ya kikao cha 73 cha dharura cha Kundi la Mawaziri wa Mambo ya Nje na Uongozi wa Kidemokrasia (CMAG), kilichofanyika Julai 10, 2026, chini ya uenyekiti mpya wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulaya wa Malta, Chris Fearne.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amejibu hawajapata taarifa rasmi kutoka Jumuiya ya Madola, ikiwafikia watajibu kama Serikali.
“Tuanasubiri kukiwa na official communication na ikafika serikalini watajibu kama Serikali,” amesema Msigwa

Hatua hiyo inakuja, ikiwa ni miezi mitatu tangu jumuiya hiyo, ilipotuma ujumbe wake nchini ulioongozwa na Rais mstaafu wa Malawi, Lazarus Chakwera, baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025 yaliyosababisha mauaji ya watu na uharibifu wa mali na kukuitana na viongozi na taasisi mbalimbali.


Ajenda ya ufuatiliaji

Katika taarifa yake ya Julai 10, 2026, Jumuiya ya Madola kupitia Kundi la Mawaziri wa Mambo ya Nje na Uongozi wa Kidemokrasia, imeeleza imeiweka Tanzania katika ajenda rasmi ya ufuatiliaji.

Pia, Jumuiya ya Madola imeelekeza hatua zaidi zichukuliwe katika maeneo kadhaa yanayohusiana na demokrasia, haki za binadamu na maridhiano ya kisiasa.

Katika kikao chake cha Julai 10, 2026, CMAG ilipokea na kujadili ripoti ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kuhusu ziara ya Chakwera nchini Tanzania na ilipokea taarifa ya maendeleo ya mchakato wa usuluhishi na mazungumzo, unaoratibiwa na ofisi ya katibu mkuu wa kumuiya hiyo.

Kwa upande mmoja, CMAG iliipongeza Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano iliotoa kwa Chakwera, ikisema ilirahisisha upatikanaji wa taarifa na mawasiliano huru katika maeneo ya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar, jambo ambalo limetajwa kuwa hatua muhimu ya kujenga imani miongoni mwa wadau mbalimbali.

Pia, kundi hilo lilibainisha kuwa limepokea taarifa kuhusu ripoti ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Serikali pamoja na tamko la Serikali la kuendelea na mchakato wa maridhiano, mageuzi na uwajibikaji.

Hata hivyo, CMAG ilieleza wasiwasi wake kuhusu kasi ya utekelezaji wa baadhi ya masuala yaliyoainishwa katika kikao chake cha 71 kilichofanyika Desemba 5, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kati ya masharti manne yaliyowekwa awali, moja limetekelezwa kikamilifu, jingine limetekelezwa kwa sehemu, huku mawili yakiwa hayajapatiwa ufumbuzi.

Kundi hilo pia, limesema hali imeendelea kuzorota tangu ziara ya Chakwere kufanyika, likitaja kuwepo kwa vizuizi vya shughuli za kisiasa nchini, shinikizo dhidi ya asasi za kiraia, vyombo vya habari na baadhi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Aidha, CMAG imeeleza kuwa bado ina wasiwasi kuhusu kuendelea kushikiliwa na kufunguliwa mashtaka kwa kiongozi mkuu wa upinzani, Tundu Lissu na hali ya hofu miongoni mwa vyama vya upinzani.

Kutokana na hali hiyo, CMAG imesema itaendelea kuiweka Tanzania katika ajenda yake rasmi na kumhimiza Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha kunakuwa na maendeleo ya dhahiri katika masuala matatu ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi.

Masuala hayo ni kuondolewa kwa vikwazo vinavyoathiri uhuru wa kukusanyika, uhuru wa kujieleza, shughuli za asasi za kiraia na vyombo vya habari.

Nyingine, ilisema ni kufanyika kwa jukwaa la mashauriano ya vyama vya siasa ili kufikia mwafaka kuhusu mwelekeo wa uchaguzi ujao.

Suala lingine, taarifa hiyo imesema ni utekelezaji wa michakato ya kisheria na kiutawala iliyo wazi kwa ajili ya kuwawajibisha wahusika wa matukio ya vurugu pamoja na kuwafidia waathirika pale inapostahili.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, ndani ya siku 30 Jumuiya ya Madola imeitaka Serikali kutafuta suluhisho la kisiasa na kisheria kuhusu suala la Lissu na kuwaachia huru watu wengine wanaoshikiliwa kwa sababu ya kutumia haki zao za msingi kwa njia za amani.

Ndani ya siku 60, Tanzania imetakiwa kurejesha upatikanaji kamili wa majukwaa ya kidijitali na kusitisha vitendo vya vitisho dhidi ya vyombo vya habari na watetezi wa uhuru wa kujieleza.

Pia, ndani ya siku 90 imetakiwa kuitishwa kwa jukwaa shirikishi la vyama vya siasa lenye usimamizi huru ili kujadili mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, ushindani wa kisiasa, suala la wafungwa na washtakiwa wa kisiasa na masuala ya uwajibikaji.

CMAG pia, imeitaka Tanzania kuanza mara moja uchunguzi huru wa jinai uliopendekezwa na Tume ya Jaji Chande na kuandaa utaratibu wa fidia kwa waathirika ukiwa na vigezo, vyanzo vya fedha na ratiba ya utekelezaji iliyo wazi.

Katika uamuzi wake, CMAG imeeleza kuwa itafanya kikao kingine cha dharura Septemba 2026 na kuialika Tanzania kuwasilisha taarifa ya maendeleo katika utekelezaji.

Aidha, Jumuiya ya Madola imesema Sekretarieti yake iko tayari kutoa msaada wa kitaalamu kwa Tanzania endapo Serikali itaomba, huku ikihimiza ushirikiano wa karibu kati ya Jumuiya ya Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono juhudi za kutafuta suluhu ya kudumu.

CMAG pia imemtaka Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na wananchi wa Tanzania na kuwasilisha taarifa zaidi kuhusu maendeleo yatakayopatikana.


Ziara ya Chakwera Tanzania

Rais mstaafu wa Malawi na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Dk Lazarus Chakwera, alifanya ziara ya kikazi nchini Tanzania Aprili 9, 2026, ambapo alikutana na viongozi na makundi kadhaa kujadili masuala ya amani, demokrasia na utatuzi wa migogoro baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Katika ziara hiyo, alikutana na Rais Samia Suluhu Hassan, mawaziri Mahmoud Thabit Kombo wa Mambo ya Nje na Profesa Palamagamba Kabudi wa Katiba na Sheria.

Pia alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro, Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu, Mbunge wa zamani wa Kisesa, Luhaga Mpina wa ACT Wazalendo pamoja na Tume ya Uchunguzi kuhusu matukio ya vurugu za baada ya uchaguzi iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Mohamed Othman Chande.

Mbali na viongozi hao, Dk Chakwera alikutana na vyama vya Chadema, ACT–Wazalendo, NLD, UDP, NCCR Mageuzi, Chama SAU, ADC, AAFP, ADA-Tadea, DP, TLP, UMD, UPDP, CCK, Demokrasia Makini na Chauma

Pia, alifanya mazungumzo na, Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jaji George Joseph Kazi, pamoja na viongozi wa Jumuiya za Kiraia (NGOs).