Tanzania, Kenya na Uganda kuunganisha nguvu za nishati
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.
Muktasari:
- Lengo la kufanya hivyo ni kupeleka ahueni ya upatikanaji wa bidhaa hiyo na kufanya bei za nishati kutokuwa na maumivu kwa wananchi
Dodoma. Migogoro inayoendelea katika nchi za Mashariki ya mbali, imeziamsha baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ambazo zimeanzisha ushirikiano wa kikanda wa mafuta na gesi ili kukabiliana na changamoto za uhaba wa bidhaa hizo.
Lengo la kufanya hivyo ni kupeleka ahueni ya upatikanaji wa bidhaa hiyo na kufanya bei za nishati kutokuwa na maumivu kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Juni 23,2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura), Charles Sangweni, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.
Mkurugenzi amesema ushirikiano huo umejikita katika kuwezesha nchi wanachama kutumia na kugawana rasilimali za nishati zilizopo katika ukanda huo ambapo itapunguza athari zinazotokana na misukosuko ya soko la Kimataifa.
Sangweni amesema Uganda na Kenya zimebarikiwa kuwa na mafuta, huku Tanzania ikiwa na gesi asilia, jambo linalotoa fursa kwa nchi hizo kuwa na ushirikiana ili kurahisisha upatikanaji wa nishati kwa wananchi wao.
Amesema rasilimali hizo zitatumika kwa ushirikiano na mgawanyo mzuri na utawezesha nchi za Afrika Mashariki kukabiliana na changamoto za mafuta na gesi inapitokea migogoro ya kimataifa.
"Kwa upande wetu Tanzania tumekuwa tukifanya shughuli za utafutaji wa mafuta tangu mwaka 1952 na hadi sasa visima 97 vimechimbwa katika maeneo mbalimbali nchini na vimetoa matokeo mazuri," amesema Sangweni.
Kuhusu ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo, amesema PURA inasimamia utekelezaji wa sera za kuwajengea uwezo wazawa na kunufaika na shughuli za mafuta na gesi.
Mkurugenzi amesema Pura itaendelea kuhakikisha haki, usawa na ubora vinazingatiwa katika usimamizi wa shughuli za mafuta na gesi nchini ili sekta hiyo ichangie zaidi katika maendeleo ya uchumi wa taifa.