Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bomba jipya kusafirisha gesi asilia kujengwa

Muktasari:

  • TPDC inapanga kuwekeza Sh120 bilioni kujenga bomba la gesi asilia la kilomita 32 kutoka Ntorya hadi Madimba, Mtwara. Mradi huo utachukua miezi minane na unalenga kuongeza nishati safi nchini.

Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linapanga kuwekeza Sh120 bilioni katika ujenzi wa bomba la gesi asilia lenye urefu wa kilomita 32 litakalounganisha kisima cha gesi cha Ntorya na Kiwanda cha Kusafisha Gesi cha Madimba kilichopo Mtwara.

Mradi huo, unaofadhiliwa na Serikali, unalenga kuongeza upatikanaji wa nishati ya gesi nchini na kusaidia mabadiliko ya nchi kuelekea kwenye vyanzo safi vya umeme.

Kampuni kutoka China za China Petroleum Pipeline na China Petroleum Technology & Development Corporation, ndizo zilizopata kandarasi ya kutoa huduma za usanifu, ununuzi wa vifaa na ujenzi (EPC) wa bomba hilo, huku ujenzi unatarajiwa kuchukua miezi minane.

“Mradi uko tayari kuanza. Tumepata wakandarasi na tumekamilisha tathmini za kifundi pamoja na fidia,” amesema Mtaalamu wa Jiolojia wa TPDC, Erick Kivera, katika mahojiano na Mwananchi leo, Julai 8, 2025.

TPDC imelipa fidia ya jumla ya Sh490.2 milioni kwa watu 255 waliotoa maeneo yao kupisha njia ya bomba hilo, wakati ambapo tathmini za athari kwa mazingira na upembuzi yakinifu pia zimekamilika.

Kisima cha gesi cha Ntorya kipo katika eneo la kimkakati karibu na miradi mikubwa ya gesi ya kimiminika (LNG).

Kampuni ya Uingereza iliyoorodheshwa kwenye soko la hisa, Aminex, inamiliki asilimia 25 ya hisa zisizo za uendeshaji katika mradi wa Ntorya.

Mradi huo unatarajiwa kusaidia kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati nchini Tanzania na kusaidia juhudi za Serikali za kupunguza umasikini wa nishati.

Katika hatua nyingine, kampuni binafsi ya nishati, ARA Petroleum, inajiandaa kuchimba kisima kipya cha gesi katika eneo la Ntorya na kuboresha visima viwili vilivyopo.

Gesi itakayopatikana kutoka kwenye visima hivyo itapelekwa katika Kiwanda cha Madimba kupitia bomba jipya.

“Sekta binafsi inaongoza kazi ya uchimbaji, wakati TPDC inaangazia ujenzi wa bomba kuhakikisha gesi inafika Madimba.

“Vipimo vitafanyika kwenye visima viwili vya sasa ili kubaini kama gesi inaweza kuchakatwa moja kwa moja Madimba au kama kutahitajika kituo kidogo cha awali cha usafishaji. Gesi asilia mara nyingi huwa na unyevu, hivyo inaweza kuhitaji kusafishwa zaidi,” amesema.

Hilo linaelezwa ikiwa ni siku chache tangu TPDC na Energetech-Tantel kusaini hati ya makubaliano (MoU) kwa ajili ya kuanza usindikaji na usambazaji wa gesi asilia nchini kote.

Mkataba huo unabeba mpango kazi wa miaka miwili unaojumuisha tafiti, vibali muhimu, uhandisi wa kina, upatikanaji wa fedha, na hatimaye, uzalishaji wa kimiminika cha gesi (LNG).

Kamishna wa Petroli na Gesi kutoka Wizara ya Nishati Tanzania, Goodluck Shirima, amesema uwekezaji wa sekta binafsi ni muhimu, kwani unatoa suluhisho zinazoweza kutumika kuendeleza viwanda vya Tanzania.

Uzalishaji wa kwanza wa LNG unatarajiwa ndani ya miezi 12 ijayo kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa.

“Kipaumbele chetu ni kuendeleza matumizi ya ndani ya gesi. Baada ya kuanza kazi, kaya na viwanda vya Tanzania vitafaidika na nishati safi ya gesi, na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji,” amesema.