Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania kufungua vituo 100 vya kufundisha Kiswahili duniani, Profesa Kabudi aja na mpya

Muktasari:

  • Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 akieleza mikakati mbalimbali itakayotekelezwa, ikiwemo kufungua vituo 100 vya kufundisha lugha ya Kiswahili duniani.

Dodoma. Wakati Serikali ya Tanzania imesema itafungua vituo 100 vya kufundisha Kiswahili kote duniani, Mbunge wa Kilosa (CCM), Profesa Palamagamba Kabudi ameonya Tanzania isijidangaye kuwa ndio nchi pekee yenye Kiswahili sanifu na fasaha.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema hayo leo Alhamisi, Mei 23, 2024 alipowasilisha bungeni maombi ya fedha Sh285.3 bilioni mwaka wa fedha 2024/2025. Wizara hiyo mwaka wa fedha 2023/2024 iliidhinishiwa na Bunge Sh35.4 bilioni.

Fedha za miradi ya maendeleo zimeongezeka kwa asilimia 2,082 kutoka Sh11.8 bilioni hadi Sh258.2 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025.


Kufundisha Kiswahili

Akizungumzia suala la Kiswahili, Waziri Ndumbaro amesema: “Kufungua vituo 100 vya ufundishaji Kiswahili kote duniani kwa kushirikiana na diaspora, lengo ni kukuza, kueneza na kubidhaisha zaidi Kiswahili.”

Kufuatia mpango huo, alipopata fursa ya kuchangia mjadala wa bajeti hiyo, Profesa Kabudi amesema “licha ya Tanzania kuwa kinara wa lugha ya Kiswaili ila tusijidanganye kuwa ndio pekee yenye Kiswahili sanifu na fasaha.”

Profesa Kabudi amezitaja nchi za Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Burundi na Rwanda kwamba kuna wazungumzaji wazuri wa lugha hiyo.

“Na nchi jirani wameanza kutumia hilo, kwamba Tanzania sasa hawazungumzi Kiswahili sanifu na fasaha, kwa hiyo msipeleke wanafunzi wenu wanaofanya mazoezi ya kujifunza Kiswahili cha kusema, cha kusoma na kuandika, kwa sababu wao wameanza kukiharibu,” amesema.

Amesema ili kubaki kuwa kinara, inabidi kushughulikia vihatarishi vitatu ambavyo vimeanza kujitokeza, ambavyo visivyofanyiwa kazi vitaporomosha umaarufu na ukinara wa Tanzania kwa kubananga Kiswahili.

“Imezuka hulka sijui imetoka wapi ya kudondosha ‘h’, huyu amekuwa uyu, huyo amekuwa uyo, kwa miaka mingi tatizo hili limekuwa la Kaskazini Magharibi ya Tanzania lakini limehama na kutamalaki Tanzania nzima.”

Profesa Kabudi ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kutumia vyombo vya habari — redio za kijamii na televisheni kusahihisha ubanangaji wa lugha, pia ametaja kihatarishi kinginge kuwa ni mtindo wa kufubaza Kiswahili.

Akifafanua, amesema: “Maneno mengi ya matumizi ya kawaida kwa sababu ya kufikiria ngono, ngono, tumeyapa maana isiyo yenyewe na matokeo yake tumeyaondoa katika matumizi ya kawaida. Badala ya matiti tunasema nyonyo, toka lini neno matiti lilikuwa baya, lakini kwa sababu tunafikiri visivyofikirika tunaanza kuondoa maneno ya Kiswahili na kuyafubaza,” alisema.

Ili Tanzania iendelee kubaki kuwa kinara wa Kiswahili, alisema “tushughulikie vihatarishi hivyo.

Profesa Kabudi hata hivyo, amesema hakatai maendeleo ya lugha na ametoa mfano wa neno fisadi kwamba kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili sanifu maana yake ni ‘mtongozaji, mharibifu, mpotovu, mwasherati, mbadhirifu, habithi lakini kwa sababu ya maendeleo ya lugha, limekuja neno jipya yaani mfujaji wa mali.

“Nilipata shida kutumia neno fisadi kwa sababu katika Biblia Takatifu neno fisadi maana yake ni mtogonzaji, msumbufu kwa wanawake wajane na vigoli, lakini leo tukubali kwamba neno hilo limepata maana mpya,” amesema.

    

Mpango wa wizara

Dk Ndumbaro amesema miongoni mwa vipaumbele vya wizara ni kufungua vituo 100 vya kufundisha Kiswahili duniani kote.

Amesema Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) liliendesha mtihani kupima umahiri wa lugha kwa wageni 49 walioingia nchini kwa malengo mbalimbali ikiwamo kufanya kazi, biashara na shughuli za kidiplomasia.

“Miongoni mwa wageni waliofanya mitihani hiyo ni madaktari 23 kutoka Afrika Kusini, Angola, Comoro, Ghana, Nigeria, Uganda na Zimbabwe.

“Aidha, mabalozi, maofisa wa ubalozini na raia wengine 10 wa nchi za Denmark, Italia, Jamhuri ya Cheki; Polandi, Uingereza, na Uswisi walifanya mtihani huo,” amesema.

Amesema pia Bakita iliendesha mafunzo ya Kiswahili kwa wageni 20 wakiwamo mabalozi wa nchi za Uturuki, Misri na Zambia hapa nchini, wageni wengine waliohudhuria mafunzo hayo nje ya mabalozi, ni raia kutoka Angola, Algeria, Marekani, Uingereza, Scotland, Denmark, Zimbabwe, na Comoro.

“Pia, Bakita iliendelea kuimarisha na kusimamia mfumo wa SwahiliPrime wa kufundisha Kiswahili kwa wageni kwa njia ya mtandao ambapo hadi Aprili,2024 wanafunzi 100,000 waliingia kwenye mfumo wa kujifunza Kiswahili,” amesema.

Amesema wanafunzi walioingia katika mfumo walitoka Marekani, Tanzania, Kenya, Uganda, Uingereza, Ujerumani, Vietnamu, Afrika Kusini, Ugiriki, Canada, India na Zambia.


Maoni ya Kamati

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, mwenyekiti wake, Husna Sekiboko, amesema wameishauri Bakita iweke mikakati ya makusudi ya kubidhaisha lugha ya Kiswahili kwa kuzalisha wakalimani wengi ambao wanatakuwa na uwezo wa kufahamu lugha zaidi ya moja kwa ufasaha, ikiwa ni pamoja na kuongeza nyenzo muhimu za kufundishia.

“Ili kufanikisha hili, Serikali ianzishe dawati la Kiswahili katika kila Ubalozi kama wenzetu China wanavyofanya.

“Aidha, katika kuimarisha matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu kwa waandishi wa Kiswahili kitaifa, kikanda na kimataifa, Kamati inasisitiza kuwa, wizara itumie balozi zetu kujenga ushawishi wa vyuo vikuu vya nje ya nchi pamoja na taasisi zingine kufundisha Kiswahili kama somo katika vyuo na taasisi hizo,” amesema.

Pia, amesema Serikali iongeze Bajeti ya Bakita ili kuongeza kasi ya kubidhaisha Kiswahili ndani na nje ya nchi.