Tanzania kuimarisha usalama mtandaoni kuelekea uchumi wa kidigitali

Muktasari:

Imeelezwa kuwa masuala ya usalama wa mtandao yana uhusiano mkubwa na masuala ya uwekezaji na uchumi

Arusha. Tanzania imeendelea kujiimarisha kuelekea uchumi wa kidigitali kwa kuongeza nguvu kwenye usalama wa mitandao kwa ajili ya kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji zaidi.

Hayo yameelezwa leo Aprili 4, 2024 kwenye Jukwaa la Tatu la Usalama wa Mtandao uliokutanisha wataalamu na wadau wa mambo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) nchini; na wa kutoka mataifa ya Ujerumani na Uswisi kujadili changamoto na kupata uzoefu wa namna ya kuboresha usalama wa kimtandao.

Mkurugenzi Mkuu Tume ya Tehama Tanzania, Dk Moses Nkundwe amesema lengo la jukwaa hilo ni kuona namna Tanzania inavyoweza kuwa salama zaidi kwenye kwenye mambo ya kijamii na biashara bila kudukuliwa na wahalifu.

“Uwezo wa nchi kulinda anga lake la kimtandao na kusaidia watu kufanya shughuli zao huko kwa uhuru bila woga wa kuibiwa wala kudukuliwa ndio njia pekee itakayoleta manufaa kwenye azma ya nchi kufikia kile kiwago cha uchumi wa kidigitali, ndio maana tunazidi kuwekeza nguvu kubwa katika hilo,” amesema Dk Nkundwe.

Amesema masuala ya usalama wa mtandao yana uhusiano mkubwa na masuala ya uwekezaji na uchumi kwa kuwa, ndio itakayovutia wafanyabiashara kutokana na kutokuwa na wasiwasi na taarifa zao, ndiyo maana wamekutana katika jukwaa hilo kujua changamoto na namna ya kutatua kwa pamoja.

“Kama mnavyojua tuko kwenye maandalizi ya kuipeleka Tanzania kwenye mapinduzi ya kidigitali ndiyo maana Tume ya Tehama tuna jukumu la kuimarisha msingi wa uchumi kama inavyotakiwa maana tumeona kuna wawekezaji wengi wakubwa wa nje wana hamu ya kuja kuwekeza Tanzania,” amesema Dk Nkundwe.

Mweyekiti wa Bodi ya Tume ya Tehama, Professa Leonard Mselle amesema usalama wa mtandao umekuwa ajenda muhimu kutokana na mfumo mzima wa maisha kuegemea huko.

“Masuala ya taarifa zetu za kiusalama yako katika mfumo wa kidigitali hasa shughuli zetu zote za kimaisha,” amesema Mselle.

Amesema kutokana na hilo, lazima kuhakikisha maisha ya watu yako salama, pesa zao ziko salama na data ziko salama. 

Mshiriki katika jukwaa hilo, Mhadhiri Msaidizi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Sakina Msonde amesema ulinzi wa kimtandao ni muhimu hasa kwa wanawake ambao ndio waathirika wakubwa wa ukatili wa kimtandao.

“Hii ni fursa kubwa sana zaidi kwa wanawake hasa katika mambo yetu binafsi ambayo watu wanatumia picha zetu kwenye mitandao ya kijamii, lakini pia jukwaa hili lituongezee kuona namna tunaweza kusaidia nchi yetu kwenye masuala ya kiuchumi,” amesema Msonde.

Ametumia nafasi hiyo kuomba Serikali kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu namna wanavyoweza kulinda usalama wa kimtandao.