Tanzania kumpa ubalozi wa heshima Sanjay Dutt

Mkurugenzi wa kampuni ya Africab Group Tanzania, Yusuf Hatimali akimtambulisha msanii wa filamu kutoka India, Sanjay Dutt anayetarajiwa kuwa balozi wa heshima Tanzania.

Muktasari:

  • Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeeleza sababu ya kumwandaa msanii wa filamu kutoka nchini India, Sanjay Dutt kuwa balozi wa heshima, kuwa ni kupenya kwenye sokjo la utalii la nchini India na Bara la Asia kwa ujumla.

Dar es Salaam. Serikali imeeleza sababu ya kumwandaa kuwa balozi wa heshima msanii wa filamu kutoka nchini India, Sanjay Dutt kutokana na mapenzi yake kwa nchi na kuwa na wafuasi wengi watakaoona na kusikia kuhusu fursa za utalii nchini.

Hayo yameelezwa jana Septemba 18 na Mkurugenzi wa Utalii wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Thereza Mugobi baada ya kumpokea msanii huyo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam.

Amesema lengo la kumchagua Dutt ni kuingia kwenye soko la India yenye idadi ya zaidi ya watu 1.4 bilioni.

“Msanii huyu ni mkubwa nchini India, ukifuatilia mitandao yake ya kijamii ana wafuasi zaidi ya 200 milioni. Kwa hiyo akituma kuhusu Tanzania, fikiria kuhusu wafuasi wote hao na siyo Wahindi peke yake bali pia ni dunia nzima, hata mimi pia ni mfuasi wake. Hivyo tunaamini kwamba kituo cha Tanzania kitasikika katika soko la India na soko kubwa la Asia, ambako pia tunalenga kufikia huko,” amesema.

Maelezo hayo yameungwa mkono na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Damas Mfugale akisema kwa kumchagua msanii huyo watafanikiwa kupenya kwenye soko la utalii la India.

“India ina idadi ya watu 1.4 bilioni na ni soko la watu wanaopoenda utalii. Takwimu zinaonyesha kuwa kuna watu milioni 200 wanasafiri kwenda nje kweye maeneo mbalimbali, kwa hiyo tumeliona kama ni soko la kimkakati.

“Huyu kuwa balozi wetu katika kutuwakilisha kama wananchi ni fursa kubwa kwetu. Tumeweka malengo kuwa ifikapo mwaka 2025 tunatakiwa tuwe tumefikisha watalii milioni tano, kwa hiyo katika kipindi cha miaka mwili mitatu ijayo tukiongeza watalii milioni 1.5 kutoka India tutakuwa tumefikisha malengo,” amesema.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), idadi ya watalii kutoka nje ya nchi waliotembelea vivutio mbalimbali vya utalii katika kipindi cha Januari hadi Mei 2022 wameendelea kuongezeka hadi 458,048 ikilinganishwa na watalii 317,270 walioingia nchini kipindi kama hicho mwaka 2021, ikiwa ni sawa na asilimia 44.4.

Akizungumzia ujio wake, msaanii huyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira wezeshi ya utalii na amekubali ombi la kuwa balozi wa heshima kwa kuwa anaipenda Tanzania.

“Nimekuwa nikija Tanzania kwa miaka 30 iliyopita, nakuja kila mwaka, naipenda hii nchi. Sikuwahi kuitangaza hii kwa miaka yote lakini kwa sasa nitaitangaza Tanzania sana na nitaitambulisha kwa mashabiki wangu, watu wa nchi yangu na watu wengine wote duiani,” amesema.

Amesema mbali na maeneo maarufu kwa utalii kama hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro, anakusudia pia kutangaza maeneo mapya kama Katavi na Ruaha.

Mmoja wa wenyeji wa msanii huyo ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Africab Group Tanzania, Yusuf Hatimali amesema ujio wa msanii huyo ni matokeo ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ya kutangaza utalii duniani.

“Kwa hiyo matunda yote haya ni kutokana na filamu ya Royal tour, ndio tunaona msanii huyu amekuja Tanzania. Kwa kuwa ana wafuasi wengi, ataziweka utalii wetu kwenye Instagram watu wote duniani wataona, kwa hiyo atatusaidia Watanzania,” amesema.