Tanzania kupokea chanjo 500,000 za Pfizer mwisho wa Oktoba

Sunday October 17 2021
Chanjo pc

Msemaji wa Serikali, Gerson Msingwa

By Mgongo Kaitira

Mwanza. Serikali imesema mwisho wa mwezi Oktoba, 2021 inatarajia kupokea dozi 500,000 za chanjo aina ya Pfizer ili kusaidia mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona nchini.

Akizungumza leo Jumapili, Oktoba 17, 2021 alipokuwa akitoa taarifa ya wiki ya Serikali jijini Mwanza Msemaji wa Serikali, Gerson Msingwa amesema chanjo hizo ni sehemu ya chanjo milioni 1.8 zinazotarajiwa kuletwa nchini kupitia mpango Shirika la Afya Duniani (WHO) unaolenga kusaidia mapambano dhidi ya vurusi hivyo katika nchi zinazoendelea.

Msigwa amesema hadi Oktoba 15 mwaka huu Watanzania 940,000 walikuwa wamepatiwa chanjo aina ya Johnson and Johnson nchi nzima.

"WHO wanatoa chanjo ili kusaidia angalau asilimia 20 ya watu katika nchi waweze kupatiwa chanjo hizi na hivi karibuni tumepokea chanjo aina ya Sinopharm ambayo kila mtu anatakiww kuchanja mara mbili na zimeshaanza kufika katika kila halmashauri," amesema Msingwa

Amewataka wananchi kujitokeza kupatiwa chanjo ya ugonjwa huo ili kujilinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Advertisement