Tanzania kusaka fursa za madini Afrika kusini

Waziri wa Madini Anthony Mavunde akizungumza katika kikao na wadau wa madini uliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Wadau wa sekta ya madini wameandaa sauti ya pamoja katika kongamano la kimataifa la madini ‘Indaba Mining Conference’ litakalofanyika Cape Town, nchini Afrika Kusini kuanzia Februari 3 hadi 8, 2024. 

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kuongeza idadi ya kampuni mpya za utafiti na uchimbaji madini pamoja na ubia kwenye kampuni za huduma na usambazaji wa bidhaa katika sekta hiyo kupitia ushawishi wa kongamano la kimataifa la madini lijulikanalo kama ‘Indaba Mining Conference’ linalofanyika nchini Afrika Kusini.

Katika juhudi za uwekezaji mpya, tayari Serikali imeshaingia mikataba na kampuni tisa zenye ubia wa asilimia 16 katika madini mkakati na muhimu hadi kufikia Novemba mwaka jana chini ya marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2017.

Mbali na masuala hayo, pia Serikali inatarajia kuongeza ushawishi wa viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa pamoja na mnyororo wa thamani kwenye sekta hiyo kwa lengo la kuchochea zaidi ukuaji na mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa kutoka asilimia 15 ya sasa. 

Kuhusu uongezaji thamani, Serikali itashawishi uwekezaji wa viwanda vya bidhaa mbalimbali ikiwamo vya helium (gesi ya kuchomea vyuma), kyanite, nikeli (bodi za magari), rare-earth element (vigae), molybdenum (vyuma vizito), lead na graphite (betri za magari) na lithium (betri za simu, labtop).    

Akizungumza leo Januari 25, 2024 wakati wa mkutano wa kujadili mawazo ya pamoja katika ushiriki wa kongamano hilo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema matumaini ya kufanikisha mipango hiyo inahusisha utayari wa kampuni zaidi ya 20 zilizojisajili kushiriki kwa sauti moja kwenye kongamano hilo. 

Kwa mujibu wa tovuti ya kongamano hilo linalotimiza miaka 30 ya kuanzishwa kwake, zaidi ya wawekezaji 900, kampuni zaidi ya 700, kampuni 470 changa na washiriki zaidi ya 8,100 wamejisajili kushiriki kongamano hilo kuanzia Februari 3 hadi 8, 2024, Cape Town, nchini humo. 

Mavunde amesema hatua hiyo itasaidia utekelezaji wa Dira ya Mwaka 2030 inayokusudia kuwekeza katika tafiti za ukusanyaji wa taarifa za viashiria vya madini mbalimbali nchini. 

“Tanzania imekuwa ikishiriki kila mwaka kwenye kongamano hilo kupitia uwakilishi wa wadau wa sekta hiyo na kila mmoja kushiriki kwa maslahi yake binafsi.Tunapishana kwenye kolido tu huko, lakini mwaka huu wote tunakwenda na malengo ya pamoja ili kuitangaza Tanzania kidunia,” amesema Mavunde.

 “Tutatangaza eneo la utoaji huduma na usambazaji wa bidhaa. Kuna mataifa yamejiimarisha zaidi katika eneo hili kuliko eneo la kodi na tozo.

“Kwa upande wetu, fedha inazokusanya Serikali katika tozo na kodi ni ndogo ikilinganishwa na mapato ya huduma na usambazaji wa bidhaa, hivyo tunaongeza nguvu hapo,” amesema.

Pamoja na maeneo hayo yaliyopewa kipaumbele na Serikali, mwakilishi wa kampuni ya minada ya vito vya thamani ya Tanzania World Auction, David Mponda ameshauri kongamano hilo liwe fursa ya kutangaza madini ya Tanzanite yanayopatikana nchini pekee, ili kuchochea utalii na uwekezaji.

Naye Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wanawake katika Madini Tanzania, Lightness Salema ameshauri kuwekeza pia nguvu katika ushiriki wa mwanamke kwenye sekta hiyo ikiwamo kuondoa vikwazo kandamizi.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, mwaka 2022/23 mchango wa sekta hiyo ulikuwa asilimia 9.1 ya Pato la Taifa (GDP), asilimia 15 ya mapato ya ndani, Dola bilioni 3.3 ya mauzo ya nje, mchango wa asilimia 56 ya fedha za kigeni na Dola milioni 50 kwa huduma na manunuzi ya ndani.

Awali, Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi (TCM), Filbert Rweyemamu amesema kazi zitakazofanyika kwenye kongamano hilo ni pamoja na kusambaza kitabu cha uwekezaji Tanzania kinachoonyesha fursa na mwelekeo wa Taifa kwa ujumla, kushiriki mikutano na kutangaza taarifa za miamba ya madini.