Tanzania kushawishi CAF Kiswahili kitumike mashindano ya Afcon

Muktasari:

  • Serikali imeanzisha mkakati mpya wa kupanua ajira za Kiswahili kwa kuwafundisha diaspora ili waweze kujiajiri kupitia lugha hiyo.

Dar es Salaam.  Serikali imesema inakuja kivingine katika kuhakikisha inawafikia wazungumzaji takribani milioni 500 wa Kiswahili duniani kuanzia sasa ikiwa ni pamoja na kupanua ajira za Kiswahili kwa watumiaji wake ndani nan je ya nchi.

Hatua hiyo imeelezwa leo Jumatatu Oktoba 16, 2023 na Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Damas Ndumbaro alipotembelea ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) ambapo amesema wameamua kuingia makubalino ya ufundishaji wa Kiswahili na vyuo vikuu na vituo mbalimbali vya kufundisha Kiswahili duniani huku wakiwapa ujuzi wa kufundisha lugha hiyo diaspora.

Dk Ndumbaro amesema katika kuhakikisha Kiswahili kinawafikia watu wengi zaidi, kutokana na fursa ambayo Tanzania imeipata kuandaa mashindano ya Afcon 2027 kwa kushirikiana na Uganda na Kenya, Serikali itatumia nafasi hiyo kushawishi lugha hiyo itumike katika matangazo yote ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Amesema majaribio hayo ya kukitangaza Kiswahili yataanza katika mashindano ya Afcon mwakani ambapo watapeleka Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ili kuhakikisa mechi zote zinatangazwa kwa Kiswahili na matangazo hayo yanawafikia nchi zinazoshiriki ambazo wanazungumza Kiswahili.

“Tutaongea na wenzetu wa CAF ili matangazo yote katika mashindano hayo yatumie lugha ya Kiswahili na kwa kuanzia majaribio tutafanya mwakani kwa kupelekea TBC irushe matangazo yawafikie nchi zote zinazozungumza Kiswahili,” amesema Dk Ndumbaro na kuongeza...

Serikali imejipanga Kiswahili kiingie katika lugha tano duniani kutoka lugha ya kumi ilivyo sasa, ajenda kama nchi ni kuona Kiswahili kinaingia Umoja wa Mataifa kama ilivyo kwa Umoja wa Afrika (AU) na Nchi za Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi amesema kutokana na maagizo mbalimbali ambayo yametolewa na viongozi wa Serikali baraza hilo limetekeleza kikamilifu ikiwa ni pamoja na kufungua vituo vya Kiswahili kwenye ofisi za ubalozi duniani.

Aidha amesema hivi sasa wamepeleka maombi ngazi husika wakipendekeza nchi za Uingereza, Ujerumani ili kuweza kufanya mkutano wa Idhaa za Kiswahili Duniani nje ya Tanzania.

Amesema hadi sasa nchi za Ufaransa na Uturuki na Morocco zimeleta maombi ya kupatiwa usaidizi kufundisha Kiswahili.

"Taarifa niliyoipata leo, Bulgaria wameanza kufundisha Kiswahili vyuo vikuu nchini humo," amesema Mushi.

“Tumeandaa kongoo ambayo itatusaidia kusambaza Kiswahili kwa njia ya Tehama, tukifanikisha hilo itasaidia watu wengi kujifunza Kiswahili kwa njia ya Tehama.

Hata hivyo amesema kwa sasa baraza hilo limeendelea kutumia Swahili Prime ambayo imekuwa msaada wa kujifunza kwa wageni wa rika mbalimbali, na kutoka mataifa yanayozungumza lugha tofauti.