Tanzania mbioni kuwa kinara wa viwanda Afrika Mashariki
Muktasari:
- Kupitia Sera ya Nishati ya Taifa ya mwaka 2015 na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, serikali imeweka nishati kuwa nguzo kuu ya mageuzi ya kiuchumi.
Dar es Salaam. Tanzania imeelezwa kuwa hatua chache tu kufikia kuwa kinara wa viwanda Afrika Mashariki, huku wataalamu wakibainisha kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika ndio unaoibeba nchi kuelekea mafanikio hayo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wataalamu wa uchumi na nishati wamesema kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, uwekezaji katika gesi asilia na nishati jadidifu, pamoja na sera thabiti za serikali, kumeiweka Tanzania katika nafasi ya kipekee ya kujenga uchumi wa viwanda.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Benki ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya Stanbic Tanzania, Elias Ngunangwa, amesema kuwa hatua ya Tanzania kuzalisha umeme wa ziada ni “mabadiliko ya mchezo” kwa uchumi wa nchi.
“Miundombinu ya nishati ndiyo kete ya kwanza kwenye mnyororo wa viwandani. Mara kete hiyo inapowekwa sawa, hufungua njia ya ajira, uzalishaji na ukuaji jumuishi,” amesema Ngunangwa.
Kwa mujibu wake, Tanzania ipo kwenye njia sahihi ya kuongoza Afrika Mashariki katika sekta ya viwanda, hasa baada ya kuanza kushughulikia changamoto ya muda mrefu ya upungufu wa nishati.
Kupitia Sera ya Nishati ya Taifa ya mwaka 2015 na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, serikali imeweka nishati kuwa nguzo kuu ya mageuzi ya kiuchumi.
Malengo ni kuongeza uzalishaji wa umeme kufikia megawati 10,000 ifikapo mwaka 2040, kutoka megawati takribani 2,400 zinazozalishwa sasa.
Mradi wa Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115 pekee, umeelezwa kuwa miongoni mwa miradi itakayobadilisha kabisa mfumo wa nishati nchini.
Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara umuhimu wa nishati katika maendeleo ya uchumi wa viwanda, akisema Tanzania sasa inajiandaa kuwa msafirishaji wa nishati wa kuaminika katika kanda.
“Nishati ndiyo msingi wa viwanda,” alisema Rais Samia katika moja ya hotuba zake, akibainisha kuwa ziada ya umeme nchini haitahudumia tu mahitaji ya ndani, bali pia nchi jirani.
Gesi, nishati jadidifu kuchochea viwanda
Ngunangwa amesema gesi asilia imekuwa injini muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda.
Amesema maeneo ya Songo Songo na Mnazi Bay tayari yanazalisha gesi inayotumika kuendesha viwanda vikubwa jijini Dar es Salaam na mikoa mingine.
“Gesi ni daraja muhimu kuelekea uchumi wa viwanda, huku serikali ikiendelea kuwekeza katika nishati jadidifu kama jua na upepo,” amesema.
Takwimu za Wizara ya Nishati zinaonesha Tanzania ina zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 za gesi asilia, rasilimali inayoiweka katika nafasi nzuri zaidi barani Afrika kwa maendeleo ya viwanda vinavyotumia nishati.
Aidha, Ngunangwa amesema taasisi za kifedha kama Benki ya Stanbic zimeendelea kusaidia miradi ya nishati kupitia mifumo bunifu ya kifedha, ikiwemo dhamana za kijani na ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma (PPP).
“Serikali haiwezi kutegemea mikopo pekee. PPP ni njia ya haraka ya kuleta utaalamu na mtaji katika miradi mikubwa kama ya kusafirisha umeme,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha PPP Tanzania, David Kafulila.
Tanzania yajipanga
Kwa sasa, Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Umeme ya Afrika Mashariki, ikiuza umeme na gesi wakati wa upungufu katika nchi jirani, hatua ambayo wachambuzi wanasema itaongeza ushawishi wake wa kiuchumi katika kanda.
Mchambuzi wa masuala ya nishati, Happiness Mshana, amesema nguvu ya Tanzania katika nishati itasaidia kuvutia viwanda vipya na kuimarisha biashara ya bidhaa za viwandani kupitia Mkataba wa Biashara Huru wa Afrika (AfCFTA).
“Kupitia AfCFTA, Tanzania inaweza kuwa kitovu cha viwanda kwa Afrika Mashariki kutokana na gharama nafuu na upatikanaji wa umeme wa uhakika,” amesema Mshana.
Kwa upande wake, mchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Johnson Mboya, amesema miradi ya nishati kama JNHPP na ile ya nishati jadidifu itaiweka Tanzania mbele ya majirani zake, hasa Kenya na Uganda, ambako gharama za umeme bado ni changamoto kwa ukuaji wa viwanda.
“Ukuaji wa viwanda hufuata uhakika wa nishati. Tanzania sasa ina kadi ya ushindi mikononi mwake,” amesema Mboya.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, Tanzania inaelekea kwenye zama mpya za uchumi wa viwanda, ikijikita kwenye nishati ya uhakika, miundombinu ya kisasa na sera jumuishi kwa malengo yanayobebwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.