Tanzania yaanzisha maktaba ya mtandaoni

Muktasari:
- Wanafunzi, walimu na wadau wengine wa elimu wataanza kupakua vitabu kwa urahisi baada ya Taasisi ya Elimu kufungua maktaba mtandao
Dar es Salaam. Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imeanza kutoa huduma za maktaba ya mtandao ili kuwasaidia wadau wa elimu kupata vitabu vya kiada na ziada kwa urahisi.
Kupitia maktaba hiyo, shule zote za Serikali zitapata huduma bure lakini binafsi zitalipia Sh400,000 na kupatiwa machapisho 48 ya kiada na zaidi ya 200,000 ya ziada.
Akizungumza leo Ijumaa Machi 29, 2019 Mkurugenzi wa TET, Aneth Komba amesema uzinduzi rasmi wa maktaba hiyo unatarajiwa kufanywa kesho na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako. Amesema wameshafanya majaribio katika mikoa 10 ambayo imesajili shule 6,639.
"Maktaba hii itahudumia shule zote za awali, msingi, sekondari na vyuo vya elimu na ni njia rahisi zaidi ya kuhifadhi machapisho," amesema Komba.
Amesema kwa shule zenye changamoto ya umeme tayari wameingia mkataba ya Mkurugenzi wa IPP Media, Reginald Mengi atakayesaidia kusambaza vifaa ikiwamo kompyuta zinazotumia umeme wa jua.
Awali, Mtaalamu wa IT wa taasisi hiyo, Kelvin Msangi alisema mwitikio umekua mkubwa kwa sababu watu wengi wanahitaji huduma hiyo.
"Maajabu ni kwamba mikoa ambayo tulidhani ina changamoto ya umeme wamejitokeza zaidi kuliko hata hapa Dar es Salaam kwa hiyo mahitaji ni makubwa," amesema.
Naye Mkurugenzi wa Tafiti, Taarifa na Machapisho wa taasisi hiyo, Kwangu Zabrone amesema maktaba hiyo pia itaweza kuhudumia watu binafsi.
"Watu binafsi watajisajili kama shule binafsi na wanaweza kupakua vitabu wanavyohitaji kwa ajili ya watoto wao," amesema.