Tanzania yajipanga kuzalisha megawati 10,000 za umeme ifikapo 2035

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi

Muktasari:

  • Kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), vijiji 5,481 vimeunganishiwa umeme katika kipindi cha miaka mitatu.

Dar es Salaam. Serikali imesema inafanyia kazi miradi ya vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ili Tanzania ifikie uzalishaji wa megawati 10,000 ifikapo mwaka 2035.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema hayo leo Machi 24, 2024 katika mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio katika miaka mitatu ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika mafanikio aliyoyaainisha kwenye mkutano huo, ni kwenye maeneo ya uchumi, fedha na uwekezaji; miundombinu na uchukuzi; huduma za kijamii na ulinzi na usalama.

Akielezea sekta ya nishati, Matinyi amesema uwezo wa jumla wa kuzalisha umeme nchini hivi sasa ni megawati 1,911 na kuwa kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na miradi ya vyanzo vingine inayofanyiwa kazi, Tanzania itafikia uzalishaji wa megawati 10,000 hadi mwaka 2035.

"Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kihistoria wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji kwenye bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), mradi huu utakuwa na vinu tisa vyenye uwezo wa kuzalisha megawati 235 kila kimoja na kufanya jumla ya megawati 2,115,” amesema.

Amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani, ujenzi wa bwawa hilo ulikuwa umefikia asilimia 33 na sasa umekamilika kwa asilimia 96.2.

Matinyi amesema miradi mingine ni ya ujenzi wa njia kubwa za kusafirisha umeme, ambazo zitaunganisha mikoa mbalimbali hadi nchi jirani na kuiwezesha Tanzania kuuza nishati hiyo nje ya nchi, pindi itakapozalisha umeme wa ziada.

Alizitaja nchi hizo kuwa ni Uganda, Kenya (itakayounganisha hadi Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan na Misri). Pia Zambia itakayounganisha umeme wa Tanzania na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Akizungumzia umeme vijijini, matinyi amesema kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), vijiji 5,481 vimeunganishiwa umeme katika kipindi cha miaka mitatu na sasa vijiji 11,843 (sawa na asilimia 96.14) vina nishati hiyo.

"Vitongoji 5,562 vimefikishiwa huduma ya umeme na kufikisha vitongoji

32,750 sawa na asilimia 51. Matarajio ni kwamba kabla ya mwaka 2025 kumalizika, vitongoji vingine 8,150 vitakuwa vimefikishiwa umeme," amesema.

Katika hatua nyingine, Matinyi amesema utalii ndiyo sekta inayoongoza kwa kuiletea nchi fedha za kigeni ambazo zimefikia Dola za Marekani 3.37 bilioni (Sh8 trilioni).

“Kimsingi sekta hii imemrejeshea shukrani Rais kwa juhudi zake binafsi za kutoka ofisini na kwenda kushiriki katika utengenezaji wa filamu ya The Royal Tour,” amesema.

Matinyi amesema katika kipindi cha miaka mitatu idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 walioipatia nchi Dola 1.31 bilioni hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023 walioingiza Dola 3.37 bilioni.

Amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua licha ya athari kubwa za mlipuko wa Uviko- 19, vita vya Russia na Ukraine na vya Mashariki ya Kati.

“Matatizo haya yaliutikisa uchumi wa Tanzania uliokuwa umefikia wastani wa ukuaji wa zaidi ya asilimia saba na kuushusha hadi asilimia 4.2 mwaka 2020. Hata hivyo, hivi sasa ukuaji umefikia asilimia 5.2 na Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa pato la kati,” amesema.

Kuhusu fedha za kigeni, amesema moja ya vigezo muhimu vya uimara wa uchumi wa nchi ni kuwa na akiba ya fedha za kigeni.

“Nchi yetu imejiwekea lengo la kuwa na akiba ya fedha za kigeni za kutosha kununua bidhaa nje ya nchi kwa miezi minne. Hivi sasa ina akiba ya kuweza kununua bidhaa kwa miezi minne na nusu na akiba yetu ya fedha za kigeni imefikia Dola 5.4 bilioni,” amesema.