Tanzania yaongoza kuwa na Simba, Nyati wengi Afrika
Muktasari:
- Sensa hiyo ilifanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri).
Arusha. Tanzania imeendelea kuimarisha hadhi yake katika uhifadhi wa wanyamapori baada ya matokeo ya Sensa ya Wanyamapori ya mwaka 2024/2025, kuonyesha kuwa nchi inaongoza barani Afrika kwa idadi ya simba na nyati.
Kwa mujibu wa matokeo ya sensa hiyo yaliyotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) leo Jumatano, Juni 17, 2026, Tanzania ina nyati 328,000, idadi inayoiweka kileleni barani Afrika, ikifuatiwa na Afrika Kusini yenye nyati 46,000, Msumbiji 45,000, Kenya 42,000 na Zambia 41,000.
Katika upande wa simba, Tanzania pia imeongoza kwa kuwa nao 17,200, ikifuatiwa na Afrika Kusini yenye simba 3,284, Botswana 3,064, Kenya 2,515 na Zambia 2,349.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa matokeo ya sensa hiyo jijini Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk Jublet Mjingo amesema sensa ya mwaka 2024/2025 imefanyika miaka 10 baada ya ile ya mwaka 2014/2015 na kwa mara ya kwanza, imehusisha mifumo yote ya ikolojia nchini.
Amesema kwa upande wa tembo, Tanzania inao 66,714, ikishika nafasi ya tatu barani Afrika nyuma ya Botswana yenye tembo 130,000 na Zimbabwe yenye takribani 100,000.
Hata hivyo, amesema idadi hiyo bado iko chini ikilinganishwa na mwaka 2005, wakati Tanzania ilikuwa na zaidi ya tembo 134,000.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava, amesema matokeo hayo yanapaswa kuwa chachu ya kuanzishwa kwa mjadala mpana wa kitaifa kuhusu mikakati ya kurejesha idadi ya tembo iliyopotea katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
“Tunapojivunia mafanikio ya uhifadhi na matokeo ya sensa hii, lazima pia tuanze mjadala wa kitaifa kuhusu namna ya kurejesha idadi ya tembo waliopotea kutokana na ujangili na changamoto nyingine,” amesema.
Ameongeza kuwa kushuka kwa idadi ya tembo kutoka zaidi ya 134,000 mwaka 2005 hadi 66,714 kwa sasa, ni ishara kuwa juhudi zaidi zinahitajika ili kurejesha hadhi ya Tanzania kama moja ya makazi makubwa ya tembo duniani.
Akizindua rasmi matokeo ya sensa hiyo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji amesema sensa hiyo imeonyesha mwenendo chanya wa uhifadhi wa wanyamapori katika kipindi cha muongo mmoja uliopita licha ya changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza.
Amesema kati ya spishi zilizofanyiwa tathmini, saba zimeonyesha ongezeko kubwa la idadi, 11 zimeendelea kuimarika, huku spishi moja ikionyesha kupungua, hali inayohitaji hatua za haraka za kisera na kiutendaji.
“Matokeo haya yanapaswa kutuongoza kufanya maamuzi sahihi, kupanga vipaumbele na kutekeleza mikakati madhubuti ya usimamizi wa rasilimali za wanyamapori na maendeleo ya utalii nchini,” amesema.
Dk Kijaji amesema wizara imepokea maelekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge na itaanza kuyafanyia kazi kwa lengo la kuongeza juhudi za kurejesha idadi ya tembo nchini.
Aidha, amesema ongezeko la shughuli za binadamu karibu na maeneo ya hifadhi, ikiwamo upanuzi wa kilimo, makazi na uvamizi wa shoroba za wanyamapori, linaendelea kuwa changamoto kubwa inayochochea migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Kutokana na hali hiyo, ameelekeza taasisi za uhifadhi kutumia matokeo ya sensa hiyo kuboresha mipango ya usimamizi wa hifadhi na kutafuta suluhisho endelevu la migogoro hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi, amesema mafanikio ya uhifadhi yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii, ambayo ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi wa Taifa.
Amesema ongezeko la mapato yatokanayo na utalii katika miaka ya karibuni ni ushahidi wa mchango wa moja kwa moja wa uhifadhi katika ustawi wa uchumi wa Tanzania, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya tafiti na sensa za mara kwa mara kwa ajili ya kupata takwimu sahihi zitakazosaidia maamuzi ya kisera.
Katika matokeo mengine ya sensa hiyo, Dk Mjingo amesema Tanzania ina faru 302, idadi inayoiweka katika nafasi ya tano barani Afrika nyuma ya Namibia yenye faru 2,196, Afrika Kusini 2,056, Zimbabwe 1,033 na Kenya 938.