Tanzania yapata mkopo wa Sh310 bilioni

Tanzania yapata mkopo wa Sh310 bilioni

Muktasari:

  • Tanzania imepata mkopo wa Sh310 bilioni kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi.

Dar es Salaam. Tanzania imepata mkopo wa Sh310 bilioni kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Oktoba 27, 2022 na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba baada ya ya hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo baina ya Serikali ya Tanzania na Korea Kusini katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Korea Kusini iliyopo mjini Seoul.

Tutuba amesema katika mikopo hiyo wanatarajia kujenga makao makuu ya ofisi za Nida Dodoma, kituo kikubwa cha kuchakata na kutunza takwimu na taarifa mbalimbali za vitambulisho vya taifa Kibaha na ofisi nyingine ndogo ya makao makuu ya Nida Zanizbar.

Pia amesema mkataba huo utaiwezesha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa na mfumo mpya wa kidijitali wa utunzaji kumbukumbu badala ya utunzaji wa kwenye makaratasi.

“Tunaamini utaratibu huu mpya utaleta urahisi na utaondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinatokana na kutokuwepo kwa mfumo rahisi na mzuri wa uhifadhi wa taarifa.” amesema

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassimu Majaliwa, Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Balozi wa Tanzania Nchini Korea Kusini, Balozi Togolani Mavura, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Aboud Hassan Mwinyi na baaadhi ya watendaji wengine.