Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yauza tani 600 za bidhaa eneo huru la biashara Afrika

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Ashatu Kijaji wakati wa hafla ya utoaji tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora nchini (PMAYA) katika ukumbi wa Super Dome jijini Dar es Salaam jana Desemba 17, 2023. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), umeanza kuzaa matunda baada ya kampuni nane za Kitanzania kupeleka bidhaa katika mataifa mbalimbali ya Afrika.

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Dk Ashatu Kijaji amesema zaidi ya tani 600 za bidhaa mbalimbali ikiwemo kahawa zimeuzwa nje ya nchi kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).

Amezitaja bidhaa nyingine ni pamoja na pilipili manga na nyuzi za katani.

Dk Kijaji ameeleza hayo jana usiku, Desemba 17, 2023 jijini Dar es Salaam katika hafla ya ugawaji wa tuzo za Rais kwa Wazalishaji bora (PMAYA) mwaka 2022. Tuzo hizo zimeandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) na kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ugawaji wa tuzo hizo ambao sasa ni msimu wa 17, umekuwa chachu kwa viwanda kujipima kuhusu shughuli wanazozifanya katika uzalishaji na huduma mbalimbali katika jamii.

Kabla ya kueleza hayo, Dk Kijaji amesema kwa nyakati tofauti wizara hiyo imekuwa ikiendesha mikutano na semina ya kuwajengea uwezo wadau wa biashara wa sekta binafsi wakiwemo wenye viwanda kuhusu faida na manufaa za Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika.

“Mheshimiwa mgeni rasmi (Rais Samia) juhudi hizi zimezaa matunda, kama Taifa tulichaguliwa kuwa miongoni mwa nchi saba ndani bara la Afrika tuliotakiwa kuanza kufanya biashara kwenye eneo huru la Afrika kama mfano.

“Nasimama mbele yako kukueleza tulianza kama ulivyotuelekeza Julai mwaka huu, hadi leo tayari tuna kampuni nane zinazofanya biashara katika AfCFTA kwa kutumia cheti cha uasilia cha bidhaa huru la biashara Afrika,” amesema Dk Kijaji.


Kwa mujibu wa Dk Kijaji, wameshatoa vyeti 17 vilivyowezesha kampuni hizo kupeleka bidhaa zao katika mataifa mbalimbali ya Bara la Afrika kupitia mkataba wa eneo huru la biashara la Afrika.

Dk Kijaji amesema kupitia vyeti hivyo wameshapeleka bidhaa za kahawa tani 330.88 kwenda Algeria na Morocco, nyuzi za katani 293.4 kwenda mataifa ya Nigeria, Ghawna na Misri na Morocco.

“Jitihada hizi ni endelevu, pia tumepeleka karanga zetu zaidi ya tani 100 nchini Misri na pilipili manga tani sita. Hizi ndizo bidhaa tulizoanza nazo katika eneo huru la biashara Afrika kama utekelezaji wa utayari wako (Rais Samia) na miongozo yako ili tufanikiwe,” amesema Dk Kijaji.