Kijaji Mwenyekiti Baraza la Mawaziri AfCFTA
Muktasari:
- Kongamano la pili limepitisha itifaki ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) ya Wanawake na Vijana katika biashara ambayo imekamilika chini ya usimamizi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na biashara katika Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Desemba 7, 2023.
Dk Kijaji aliongoza kikao cha 12 cha AfCFTA Desemba 7, 2023, kilichofanyika sambamba na mkutano wa pili wa AfCFTA wa Wanawake na Biashara (CWT) jijini hapa ulioanza Desemba 6 na kuhitimishwa Desemba 8, 2023.
Mkutano huo pia umepitisha Itifaki ya AfCFTA kwa wanawake na vijana katika biashara. Itifaki hii ilikamilishwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anahudumu kama mhamasishaji mkuu na kiongozi wa wanawake na vijana katika biashara barani Afrika.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema Serikali inatafuta njia za kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara wanawake chini ya AfCFTA na kubaini teknolojia zinazofaa, ili kuwaongezea uwezo wa uzalishaji.
Mpango huu utakamilishwa kwa kuimarisha mazingira wezeshi na miundombinu muhimu kwa mafanikio ya biashara zao.
"Sisi Tanzania tumeendelea kuimarisha upatikanaji wa mitaji kupitia taasisi zetu za fedha, zikiwemo benki," amesema Kigahe.
Ameongeza wizara kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), inatoa mafunzo ya ujasiriamali, mikopo ya mitaji na kuwapa fursa wanawake wajasiriamali kupata teknolojia.
Mitaji kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu pia inatengwa kupitia asilimia 10 ya mapato yanayotokana na serikali za mitaa.
“Kwenye eneo hili la mitaji kuna zile fedha zilizokuwa zinatolewa kupitia halmashauri, tutakopesha kwa akina mama, vijana na watu wenye mahitaji maalumu sababu haya ndiyo makundi tunaona yanashiriki sana katika uzalishaji na ufanyaji biashara ndogondogo zinazochangia pato la Taifa,” amesema.
Amesema eneo la biashara la Afrika lina nchi zaidi ya 55 ambazo Waafrika wanaweza kufanya biashara pamoja.
“Kuna bidhaa nyingi zinapatikana Tanzania vikiwamo viungo, vyakula na mkonge ni ambao ni bidhaa inayotumika sana katika nchi za Afrika hasa Afrika Kaskazini na Magharibi,”amesema.