Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania, Zambia kuimarisha ulinzi bomba la mafuta

Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, baada ya kumalizika kwa mkutano wa pamoja kati ya Zambia na Tanzania uliojadili kuhusu bomba la mafuta kutoka nchini hadi Zambia. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Mawaziri sita wa sekta za nishati na ulinzi wa Tanzania na Zambia, wamekubaliana mambo sita, ikiwemo kuimarisha ulinzi katika maeneo ambayo bomba la mafuta la Tazama linalosafirisha dizeli linapita.

Dar es Salaam. Mawaziri sita wa sekta za nishati na ulinzi wa Tanzania na Zambia, wamekubaliana mambo sita, ikiwemo kuimarisha ulinzi katika maeneo ambayo bomba la mafuta la Tazama linalosafirisha dizeli linapita.

Masuala mengine waliokubaliana ni pamoja na kuongeza idadi ya askari watakaolinda bomba hilo, kushirikiana jamii, kutumia ndege zisizo na rubani 'drones' na kuongeza wigo wa bomba hilo ili lisafirishe mafuta kwa ufanisi.

Mkutano huo uliofanyika leo Julai 7, umewahusisha mawaziri akiwamo Waziri wa Nishati January Makamba, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Innocent Bashungwa, wakati kwa upande wa Zambia waliwakilishwa na Waziri wa Nishati, Peter Kapala, Jacob Mwiimbu (Waziri wa Mambo ya Ndani) na Waziri wa Ulinzi, Ambrose Lufuma.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Waziri Makamba amesema wamekubaliana pia kuimarisha miundombinu ikiwemo makambi na vituo vya polisi vinaongezeka katika maeneo ya mahsusi ambayo bomba hilo linapita

"Pia tumekubaliana kuimarisha kamati za ulinzi na usalama ambapo bomba linapita, matumizi ya drones na ushirikishaji wa wananchi katika vijiji," amesema.

Amesema kikao hicho kilikuwa kikao cha mafanikio makubwa akiwashukuru viongozi Serikali ya Zambia kwa kuhudhuria mkutano huo.Alifafanua kuwa namna wanavyosimama imara kuendeleza misingi ya uhusiano kati ya mataifa hayo.

"Pamoja na suala la ulinzi tumejadili upanuzi wa bomba lenye ili kusafirisha kwa ufanisi mafuta. Pia tumejadili ujenzi wa bomba jipya la gesi," amesema Makamba ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho.

Amesema hilo lilijengwa miaka 60 ambapo lilikuwa likisafirisha mafuta ghafi yalikuwa yakisafishwa nchini, lakini kuanzia Machi mwaka huu limeanza kusafirisha dizeli sio mafuta ghafi hivyo lazima kuimarisha ulinzi.

Kwa upande wake, Lufuma amesema wamekubaliana kuimarisha ulinzi katika bomba hilo, akisema hivi sasa miundombinu hiyo inasafirisha bidhaa iliochakatwa kwa ajili ya matumizi ya mwisho.

"Hii ni bidhaa ambayo ipo tayari kwa matumizi hivyo inahitaji ulinzi wa kutosha. Hivyo tutahakikisha kuwa kunajengwa vituo vya polisi pembezoni mwa bomba hilo ili kuimarisha ulinzi," amesema.

Lufuma alisema endapo ulinzi ukiimarishwa historia ya bomba hilo itaendelezwa, akisema mpango utakwenda sambamba kuongeza pia matumizi ya teknolojia katika usafirishaji nishati hiyo.

"Kulingana na uhitaji wa mafuta uliopo Zambia, tumepanga kuongeza wigo wa bomba la sasa lenye inchi nane hadi kufikia inchi 12 na kusaidia kukidhi mahitaji yanayozidi kuongezeka," amesema na kuongeza kuwa mpango wa muda mrefu ni kupanua bomba hilo hadi kufikia inchi 24.