Tarura Rukwa yaongezwa bajeti kuboresha miundombinu ya barabara

Muktasari:

  • Tangu mwaka 1982, wakazi wa Kirando, Kazovu na Korongwe  mkoani Rukwa walikuwa na shida ya miundombinu hususan barabara, hali iliyosababisha wajawazito kushindwa kufika hospitalini kwa wakati.

Rukwa. Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) mkoani Rukwa umesema umefanikiwa kuboresha mitandao ya barabara, vivuko na madaraja baada ya Serikali kuuongezea bajeti kutoka Sh5.63 bilioni  mpaka Sh12.3 bilioni .

 Umesema fedha hizo zimeboresha barabara zenye urefu wa kilomita 2,304.26 sambamba na  madaraja 80 na vivuko vidogo 2,722.

Meneja wa Tarura  Mkoa wa Rukwa, Mhandisi William Lameck ameliambia Mwananchi Digital leo Jumatatu Aprili 15,2024 kuwa uwekezaji huo umechochea  fursa za kiuchumi kwa wananchi sambamba na kuongezeka kwa mapato ya Serikali kutokana na shughuli za kibiashara zinazoendelea kufanyika.

“Pia tumeboresha miundombinu ya  barabara za changarawe kutoka kilomita  867.25 hadi   1,143.05 zilizojengwa kwa ufanisi mkubwa  kulingana na thamani ya fedha,” amesema.

Amesema ili kuunganisha mawasiliano ya miundombinu, Serikali imeshatoa Sh1.76 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Kavunja lenye urefu wa mita 39 linalounganisha vijiji vya Kirando, Kazovu na Korongwe  katika Wilaya ya Nkasi ambalo limekamilika kwa asilimia 100 na limeanza kutumika.

Mkazi wa Kijiji cha  Kazovu, Anna Zuberi amesema tangu mwaka 1982, walikuwa na shida ya miundombinu hususan barabara, hali iliyokuwa ikisababisha hata wajawazito kushindwa kufika hospitalini kwa wakati.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutupigania tumepata barabara sambamba na kufunga  taa, zamani tulikuwa tunapata shida sana kulikuwa na madimbwi na usafiri haukuwepo,” amesema Zuberi.

Naye Shabani Mkisi mkazi wa Korongwe ameishukuru Serikali kwani barabara hiyo ya lami imewarahisishia usafiri na sasa inapitika wakati wote.