TASAC wataja chanzo cha kuzama kwa boti Coco Beach
Muktasari:
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limesema watu wote tisa wameokolewa na wanaendelea vizuri kiafya bila ya kuwa na changamoto yoyote baada ya ajali ya boti ya uvuvi MV LEGACY kuzama jana ufukwe wa ‘Coco Beach Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kukatika kwa kamba upande wa kulia wa boti ndio chanzo cha kuzama kwa boti ya uvuvi “MV LEGACY”
Kwa mujibu wa TASAC, boti hiyo yenye namba za usajili DS/L1175 ikimilikiwa na Yakoub Khamis, ilizama saa 9:50 Machi 10 karibu na ufukwe wa Coco Beach, kata ya Msasani wilayani Kinondoni Dar es Salaam ikiwa na mabaharia tisa na wavuvi sita, mhandisi mitambo mmoja na manahodha wawili.
Boti hiyo iliyopatiwa cheti cha usajili na ubora na TASAC kufanya shughuli za uvuvi Machi 6, 2024, ina urefu wa mita 11 na upana wa mita 1.7.
Taarifa iliyotolewa leo Machi 11, 2024 na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Mohamed Salum, boti hiyo ilikuwa kwenye majaribio ya kiufundi baada ya matengenezo ya mifumo ya uvuaji samaki kwa kukokota.
Kulingana na taarifa ya TASAC boti hiyo ilianza majaribio majira ya saa 3:00 asubuhi ikitokea eneo la Tandahimba, Kivukoni na kufanya majaribio ya kuvua samaki wakizunguka katika maeneo yenye maji mafupi karibu na eneo la daraja jipya la Tanzanite (Upanga) hadi Coco Beach (Oysterbay).
“Ilipofika majira ya saa 9:50 alasiri wakati nahodha anabadilisha uelekeo wa boti kuelekea upande wa kulia, ndipo kamba moja ya upande wa kushoto ikakatika na kusababisha uzito kuelemea kwenye kamba ya upande wa kulia, ndipo uzito ulipohama ghafla na kuilazimisha boti kunywa maji upande wa kulia kisha kuzama,” imeandikwa kwenye taarifa hiyo.
Baada ya tukio hilo kuripotiwa, saa 10:01 kituo chao cha kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji (MRCC) kilitoa taarifa Jeshi la Polisi (Wanamaji) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kufika eneo la tukio kwa uokoaji.
“Watu wote tisa wamefanikiwa kuokolewa na wanaendelea vizuri kiafya bila ya kuwa na changamoto yoyote, TASAC inatoa rai kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo majini kuzingatia sheria na kanuni za udhibiti usafiri majini na kuhakikisha muda wote wanavaa makoti ya uokozi ili kujiepusha na maafa yanayosababishwa na tukio la ajali,” imeandikwa kwenye taarifa hiyo.