Tasaf yatekeleza miradi 11 ya maendeleo Zanzibar

Muktasari:
- Utekelezaji wa miradi ya TASAF Zanzibar umeendelea kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu, afya na miundombinu, huku ukiwanufaisha wananchi wa Unguja na Pemba.
Zanzibar. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika kisiwa cha Unguja, Zanzibar.
Kamati hiyo imetoa pongezi hizo baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa ukumbi wa mitihani na dahalia ya wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Kizimkazi Dimbani, mkoa wa Kusini Unguja.
Dahalia hiyo ya kisasa yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 248 imelenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Akizungumza baada ya ziara hiyo leo Februari 18, 2025, Mwenyekiti wa Kamati, Florent Kyombo, amesema ujenzi wa dahalia hiyo ni kielelezo cha juhudi za kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Kizimkazi Dimbani.
“Tunaipongeza TASAF kwa kazi nzuri iliyofanyika hapa. Tumejionea mradi huu ulivyotekelezwa kwa viwango na ubora wa hali ya juu. Miradi ya aina hii ni muhimu kwani inachochea ari ya kusoma kwa wanafunzi wetu,” amesema Kyombo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, alisema utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi na kuboresha maisha yao.
“TASAF imeweza kujenga shule, madarasa, vituo vya afya, madaraja, barabara pamoja na miundombinu ya maji na umwagiliaji. Haya yote ni kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,”amesema Sangu.
Aliongeza kuwa ujenzi wa dahalia hiyo uliogharimu Shilingi milioni 336 utakuwa mkombozi kwa wanafunzi wa kike, kwani utasaidia kuboresha mahudhurio na kuongeza ufaulu wao.

Awali, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TASAF, Godwin Mkisi, alisema miradi hiyo ni sehemu ya awamu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
“Hadi kufikia Januari 2025, jumla ya miradi 14 ya miundombinu ya elimu na afya yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.3 imetekelezwa katika visiwa vya Unguja na Pemba, ambapo miradi 11 imekamilika na kukabidhiwa kwa sekta husika, huku miradi mitatu ikiendelea kutekelezwa,”amesema Mkisi.
TASAF imeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar, ikihamasisha ustawi wa jamii kupitia miradi inayolenga kuboresha huduma za msingi za elimu, afya na miundombinu.