Tatizo la Zanzibar ni vurugu za kijinai au kisiasa?

Muktasari:

Katika jamii ya watu wanaokinzana, kama inavyotokea mara kadhaa visiwani Zanzibar, ama hutokea vurugu za kisiasa au vurugu za kijinai.

Katika jamii ya watu wanaokinzana, kama inavyotokea mara kadhaa visiwani Zanzibar, ama hutokea vurugu za kisiasa au vurugu za kijinai.

Vurugu za kisiasa zina eneo, wahusika wenye wafuasi na husababishwa na masuala mengi yakiwamo ya kihistoria, jiografia, ubaguzi, itikadi na kutoaminiana.

Ni muhimu kutafakari kiini cha tatizo kwani matatizo huzidi kila yanapochelewa kutatuliwa na hayaondoki kwa kutibu dalili zake.

Ipo fikra inayoamini unyanyasaji uliokithiri na uovu uliopindukia kuwa chanzo cha vurugu za kipindi cha uchaguzi visiwani Zanzibar. Suluhisho lake, wanaamini ni kufikiria vurugu hizi kama za jinai, na kutaka uwajibishwaji wa wahusika.

Tafakuri ya kina inahitajika kujiridhisha kama yanayotokea Zanzibar yanapaswa kuzingatiwa kama masuala ya kijinai au ya kisiasa.

Kutafuta suluhisho kwa kuwawajibisha wahusika katika mahakama za jinai iwe za kitaifa au za kimataifa huenda yakawa ni matokeo ya kutotofautisha vurugu za kisiasa na za jinai.

Kisiasa, tunawekeza nguvu nyingi kutaka wahusika wawajibishwe badala ya kuzingatia masuala yanayosababisha uhasama na vurugu zinazotokea. Kwa hivyo, kutafuta ufafanuzi wa mahakama kunaweza kukuza badala ya kupunguza vurugu katika jamii kwa vile wahusika na waathirika bado wapo katika jamii.

Ni muhimu kukubali kwamba migogoro ya Zanzibar ni ya matabaka ya wenyewe kwa wenyewe hivyo maridhiano yana nafasi ya kuleta suluhu ya kudumu.

Maridhiano yalisaidia kupunguza uhasama, mgogoro na vurugu Zanzibar na yanaendelea kudhihirisha kuwa kususa na siasa tenganishi hazina msaada, zinazidisha tatizo.

Suluhu ya maana zaidi ni mageuzi ya kisiasa yanayopatikana kwa kushirikiana na kuwa sehemu ya Serikali.

Kuendelea kususia kufikiria kudai haki mahakamani kutaongeza ugumu wa mageuzi na kuzua vurugu, uhasama na mateso hivyo kuingia kwenye visasi, ubaguzi na kukomoana.

Siasa za kususa zilishafanyika Zanzibar. Jaribio la kufungua kesi za uhalifu dhidi ya ukiukwaji wa haki za binaadamu pia limewahi kufanywa lakini bado tatizo lipo na linajirudia.

Mgogoro wa Zanzibar uliodumu kwa zaidi ya nusu karne ni ngumu kupata utatuzi kwa ama kususia au kudai haki ya jinai kwa sababu tunaotaka kuwapeleka mahakamani au kuwasusia tunaowahitaji kumaliza mzozo uliopo.

Ipo haja ya kufikiria njia mpya itakayotusaidia kutofautisha haki ya jinai, haki ya kisiasa na ile ya kijamii na kuweka kipaumbele katika haki ya kisiasa ambayo ni mageuzi ya mfumo wa kisiasa.

Haki ya kisiasa inalenga jamii yote kwa mapana yake wakati haki ya jinai inalenga watu binafsi na wachache. Lengo la haki ya jinai ni adhabu wakati haki ya kisiasa inakusudia kuletani mageuzi ya kimfumo na kiutendaji kuanzia ngazi za juu za uongozi serikalini, taasisi na idara zake.

Nia njema, yenye shabaha ya kujenga utengamano wa kijamii inahitajika ikiamini uongozi ni dhamana na ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Tunahitaji kujenga utamaduni wa kuaminiana, kuachana kubaguana na maridhiano na kuwa sehemu ya Serikali si lengo bali mwanzo wa safari kuelekea Zanzibar tuitakayo.

Wahusika wa pande zote wakubaliane kuweka kanuni za Kikatiba zitakazofafanua vigezo vya kugawana madaraka kuanzia juu hadi chini, kuacha urasimu na kuviboresha vyombo vya ulinzi na usalama viwe huru vinavyowatumikia raia wote kwa usawa.

Halikadhalika, tunahitaji kuanzisha mageuzi ya uchaguzi yatakayokuwa shirikishi yatakayozalisha wapinzani wa kisiasa badala ya maadui kama wanavyoonekana sasa.

Uandaliwe muswada wa haki utakaojumuisha Wazanzibari wote katika kuajiriwa...ajira zitegemee sifa na uwezo wa mtu badala ya itikadi za kisiasa au eneo analotoka.

Ili Zanzibar ipige hatua za kimaendeleo, inahitajia mabadiliko ndani ya Serikali ambako watu watachaguliwa kwa misingi ya uwezo, upeo na sifa zao.

Wakati umefika wa vyama kubadili msimamo kwa kuacha kususia kwa gharama ya kuendeleza tatizo na kuongeza madhara kwa wananchi.

Mafanikio iwe kukubaliana mageuzi ya kisiasa yatakayoondoa ubaguzi wa kisheria na kisiasa. Shabaha isiwe kulipiza kisasi kwa waliokufa bali kuwapa walio hai nafasi ya pili.

Bado kuna machungu lakini ndio safari ya uponyaji. Tuwatakie uponyaji wa haraka majeruhi. Tuzitambue na kuzifariji familia zilizoathirika na tuwaombee waliopoteza maisha.

Katika dunia ya leo, uhusiano kati ya vyama vya siasa ni muhimu ingawa uhusiano na utengamano wa watu ndio msingi halisi wa demokrasia. Diplomasia, uongozi makini na ustawi mwema.

Uhasama na chuki havilingani na haki wala kuhamasisha uadilifu hivyo hatupaswi kuruhusu chochote kusimama kati kwani Zanzibar itaimarika zaidi kupitia ushirikiano kuliko kususia.

Wakati tunatazama yaliyopita, turekebishe kasoro zilizojitokeza kwani hatuwezi kufikiria mema ikiwa tutaendelea kuishi kwa mabaya ya zamani.

Zanzibar ni nchi yetu sote, watu wa mirengo tofauti ikiwa na utajiri mkubwa wa mchanganyiko wa makabila na asili tofauti za watu. Wazanzibari tutakuwa na nguvu na sauti licha ya udogo wa nchi yetu ikiwa tutakuwa na mfumo shirikishi.

Imeandikwa na Khalid Said Suleiman