Tatu za nguvu zaibeba God's Bridge matokeo Darasa la Saba 2020

Tatu za nguvu zaibeba God's Bridge matokeo Darasa la Saba 2020

Muktasari:

Matokeo mazuri yanatokana na mifumo ambayo walimu wanasema wamejiwekea sambamba na malezi yenye maadili sambamba na dini wanayoyapata wanafunzi shuleni hapo.

Mbeya. Uongozi wa shule ya msingi mchepuo wa Kiingereza ya God's Bridge iliyoko wilayani Rungwe mkoani Mbeya, umetaja mambo matatu yaliyowafanya waibuke na ushindi katika matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba yaliyotangazwa leo na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) nchini Tanzania.

Kaimu Mkuu wa Shule hiyo akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumamosi Novemba 22, 2020 baada ya NECTA kutangaza matokeo hayo, Gabriel Mbeli amesema juhudi za kipekee na mbinu za ufundishaji kipindi cha janga la corona, ni miongoni mwa sababu zilizotoa matokeo chanya kwa wanafunzi wao.

Amesema kipindi hicho ambacho shule zilifungwa kwa muda usiojulikana, walilazimika kuanza kuwafundisha wanafunzi hasa madarasa yaliyokuwa yanakabiliwa na mitihani ya Taifa, kwa njia ya mitandao ya kijamii, ukiwamo wa Whatsup.

“Tulikuwa tukituma maswali na masomo kwenye namba za simu za wazazi na walezi na kuwaomba wawapatie watoto wao, baada ya kusoma na kuyajibu, waliyarejesha kwetu tukawa tunasahihisha na kutoa ufafanuzi pale tunapobaini wanafunzi kutoa elewa,” amesema mwalimu huyo.

Lakini pia amesema jambo la pili ni ushirikiano wa hali na mali tulioupata kutoka kwa wazazi, walezi, wanafunzi na walimu sambamba na kumuomba Mungu.

Mbinu ya tatu amesema ilikuwa ni kufundisha kwa kupitia televisheni ambako walimu walitoa maswali kwa teknolojia za kisasa sambamba na kuwaandaa wazazi kufuatilia vipindi hivyo kila virushwapo kusudi watoto wao wahudhurie.

Anasema walimu wote shuleni hapo walifundisha wanafunzi bila kuchoka kwa dhamira moja ya kutaka wafanye vizuri katika mitihani yao ya mwisho.

“Miezi mitatu ya Covid - 19 kwetu ilikuwa sio changamoto kubwa sana katika kazi, kwa sababu kabla ya hapo  pia tulikuwa na mfumo wetu wa ufundishaji wa wanafunzi wakiwa likizo kwa njia ya kuwatumia maswali wazazi bila gharama zozote, malipo yao ilikuwa ni kununua vifurushi vya tu vya simu,” amesema makamu mkuu huyo wa shule.

Naye Mwalimu Baraka Mwakilima amesema matokeo mazuri yanatokana na mifumo ambayo walimu waliyojiwekea sambamba na malezi ya maadili ya kidini wanayoyapata wanafunzi shuleni hapo.

“Bila Mungu hakuna linalowezekana, kwa hiyo huwa tunawasisitiza sana wanafunzi wamche Mungu na wawe na bidii,” amesema Mwakilima.

Alipoulizwa nini mikakati yao baada ya matokeo haya, mwalimu huyo amesema ni  kuendelea kufanya vizuri zaidi.