TB Joshua kuzikwa siku ya 34 baada ya kifo chake
Muktasari:
Leo Ijumaa Julai 9, 2021 maelfu ya waombolezaji wamejitokeza kuaga mwili wa mhubiri maarufu duniani, Temitope Balogun Joshua maarufu TB Joshua anayezikwa leo nchini Nigeria.
Leo Ijumaa Julai 9, 2021 maelfu ya waombolezaji wamejitokeza kuaga mwili wa mhubiri maarufu duniani, Temitope Balogun Joshua maarufu TB Joshua anayezikwa leo nchini Nigeria.
TB Joshua alifariki dunia Jumamosi ya Juni 5, 2021 nchini humo akiwa na umri wa miaka 57. Ibada ya kuaga inafanyika katika kanisa Synagogue Church of All Nations (SCOAN) mjini Lagos.
Taratibu za mazishi yake zilianza kufanyika Jumatatu ikianza misa katika kanisa hilo na Jumanne waombolezaji walitoa heshima za mwisho. TB Joshua alijipatia umaarufu kutokana na kuponya watu wa mataifa mbalimbali na huduma yake kuwa maarufu duniani kote.
Evelyne ambaye ni mke wa TB Joshua na watoto wake watatu walipata fursa ya kumzungumzia maisha ya nabii huyo ambaye saa chache kabla ya kifo chake alizungumza na wasaidizi wake ambao baadaye walitoa ushuhuda kuwa alijua kifo chake na aliwaaga kutokana na kauli alizokuwa akiwatamkia.
“Kutoka kuwa na kusanyiko la waumini wanane wa kanisa hadi kuwa na kanisa lililojaa umati wa watu na kuwa na wafuasi kote duniani. Alinifunza kuwa mwanamke niliye leo. Kuwa dhahabu lazima ipitie moto. Ninataka tu kukushukuru kwa kuwa baba mwema wa watoto wetu,” amesema Evelyne.
Watoto wake TB Joshua , Sarah, Promise na Heart walimsifu baba yao kwa kuwa mtu aliyejitolea kumtumikia Mungu.
“Kwa heshima bila woga aina ya upendo uliotuonesha hatukuwahi kuuona maishani mwetu. Kama kuna mtu yeyote aliyeishi maisha ya kushangaza ni wewe. Baba yangu alikuwa na utu kwa namna ambayo sikuwahi kuelewa kamwe ," amesema Sarah.