TBS kuiondoa sokoni juisi ya Apple ‘Ceres’ inayotajwa kuwa na sumu

TBS kuiondoa sokoni juisi ya Apple ‘Ceres’ inayotajwa kuwa na sumu

Muktasari:

  • Kutokana na juisi ya tufaa ‘Apple’ iliyotengenezwa na kampuni ya Afrika Kusini ya Ceres kudaiwa kuwa na kiwango cha juu cha sumu, Tanzania imeungana na mataifa mengine saba kuiondoa sokoni.

Dar es Salaam. Kutokana na juisi ya tufaa ‘Apple’ iliyotengenezwa na kampuni ya Afrika Kusini ya Ceres kudaiwa kuwa na kiwango cha juu cha sumu, Tanzania inaungana na mataifa mengine saba kuiondoa sokoni.

Juisi hiyo toleo la Juni 14-30, 2021 imetajwa kuwa na aina ya sumu inayotokana na baadhi ya sumu kuvu katika tufaa na bidhaa zake.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 14, 2021 Mkurugenzi wa udhibiti ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Lazaro Msasalaga amesema suala hilo linafanyiwa kazi.

Amesema kila bidhaa inayoingia nchini hupimwa na hivyo ikiwa itabainika toleo hilo lipo ndani ya nchi itaondolewa haraka na utaratibu mwingine wa kuichunguza utafanyika.

“Tunalifanyia kazi, toka jana tunakusanya taarifa tuone kwamba ziliingizwa na nani kama zipo na iwapo tutazibaini utaratibu utafanyika kubaini ziliingizwa lini na nani anahusika,” amesema Msasalaga.

Amesema juisi za Ceres ni salama na hazina shida isipokuwa mtu hatakiwi kununua toleo tajwa ambapo wao ‘TBS’ wanalifuatilia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 11 na Jumuiya ya soko la pamoja la nchi za mashariki na kusini mwa Afrika (COMESA) imetaja matoleo sita yaliyotolewa kati ya Juni 14 na 30 kwa Barcode 6001240200018 (Ceres Apple 4x6x200ml).

Comesa imesema miongoni mwa maeneo ambayo yameathirika zaidi na toleo hilo ni DRC Congo, Seychellies, Zambia na Zimbabwe.