TCAA kufunga mfumo mpya wa mawasiliano ya anga

Muktasari:

  • Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, (TCAA), imesema inaanza kufunga mfumo mpya wa mawasiliano ya sauti ya anga nchi nzima ndani ya miezi 18 kuanzia sasa.

Dar es Salaam. Miezi 18 kuanzia sasa, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, (TCAA), itafunga mfumo mpya wa mawasiliano ya sauti ya anga nchini.

Kwa mujibu wa TCAA, mfumo huo mpya, ni wa kimataifa wa redio za mawasiliano ya sauti kati ya rubani na mwongoza ndege (VHF-Digital Radio), ambao unaelezwa kuwa utachagiza kuboresha sekta ya anga nchini.

Akizungumza wakati akipokea makontena tisa ya vifaa vya mfumo huo vilivyotoka nchini Norway na Italia, Mkurugenzi Mkuu mamlaka hiyo, Hamza Johari amesema mfumo uliopo sasa umepitwa na wakati ndio maana Serikali ilitoa Sh31.5 bilioni kwa ajili ya manunuzi ya mfumo mpya.

Amesema mitambo hiyo ni redio za kidijitali za masafa ya juu, mitambo ya kurekodi mifumo ya mawasiliano ya sauti pamoja na mifumo ya kuunganisha na kuangalia mifumo ya mawasiliano.

“Ndege zinazotumia anga la Tanzania zitakapotaka mawasiliano popote pale zitakapokuwa zikiiita tu basi tunasikia kupitia mitambo hii maana ni mfumo wakitaalamu unaofanya kazi nchi nzima,” amesema na kuongeza;

“Tutafunga Dar es Salaam - Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Pemba, Uwanja wa Abeid Karume Zanzibar, Songwe, Mwanza, Tabora, Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma, Tanga na Mtwara” amesema Hamza.

Mbali na viwanja hivyo amesema mfumo huo utafungwa katika vituo 18 nchini ambavyo vimefanyiwa utafiti kwa lengo la kukuza na kurefusha mawasiliono ya sauti.

Amesema mfumo huo utachagiza idadi ya miruko ya ndege pia kuchagiza mashirika ya ndege yanayokuja nchini pamoja na abiria sambamba na kuiunga mkono mradi wa Royal Tour uliopelekea kuja kwa watalii.

Katika kuutekeleza mradi huo Hamza amesema waliwapeleka wataalamu 24 nchini, Norway na Italia kwa ajili ya kupata mafunzo na sasa wamerudi tayari kwa kuanza kazi.

Aidha, Mkurugenzi Huduma za Uongozaji Ndege, Flora Mwanshinga amesema kwamba mfumo huo utabadilisha sekta kutokana na changamoto zilizokuwepo kwenye mfumo wa sasa ambao umekaa kwa muda mrefu.

“Kwa sasa kumekuwa na upanuzi na ukuaji wa sekta ya anga tunategemea mitambo hii itaboresha huduma zetu hivyo mashirika mengi zaidi yataingia nchini.

“Dunia nzima sasa inatoka kwenye mifumo ile ya zamani inaenda kwenye mifumo ya kidijitali kwahiyo tunavyoondoka kwenye mifumo ya kizamani imanaana tunakua,” amemalizia Flora.