TCRA yaja na suluhu utapeli usafirishaji vifurushi

Kaimu meneja wa TCRA Kanda ya Mashariki, Ikuja Jumanne akizungumza na wadau mbalimbali wanaotoa huduma ya usafirishaji wa vifurushi na vipeto katika kanda hiyo.

Muktasari:

  • Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka watoa huduma ya usafirishaji wa vifurushi kufuata sheria na kukata leseni kabla ya kuanza biashara hiyo ili kupunguza vitendo vya utapeli katika biashara hiyo kinachofanywa na watu wasiokuwa waaminifu.

Dar es Salaam. Ripoti ya robo mwaka unaoishia Machi 2023 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeonyesha kushuka kwa usafirishaji wa vifurushi na mizigo ndani na nje ya nchi.

Ripoti hiyo inaonyesha kwa upande wa ndani ya nchi usafirishaji huo umepungua kwa asilimia 76.3 kutoka vifurushi milioni 9.3 mwaka 2019 hadi milioni 2.2 mwaka 2022.

Huku kwa upande wa vifurushi vya kimataifa vimeshuka kutoka milioni 2.9 mwaka 2019 hadi 260,394 mwaka 2022 sawa na kushuka kwa asilimia 91. Hali hiyo inaelezwa kusababishwa na upotevu na utapeli unaofanywa wa vifurushi na vipeto wakati wa kusafirisha.

Ili kudhibiti kero hiyo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka watoa huduma hiyo kuhakikisha wanatimiza matakwa ya kisheria kwa kukata leseni kabla ya kuanza kutoa huduma hiyo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa TCRA, Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Ikuja Jumanne akizungumza katika mkutano na wadau wanaotoa huduma uliofanyika Aprili 28, 2023 jijini Dar es Salaam.

“Leseni ya kusafirisha vifurushi ni muhimu sana kwa sababu inahakikisha kuwa biashara ya usafirishaji wa bidhaa inafuata sheria na kanuni za usalama na kuongeza uaminifu wa wateja,”amesema.

Jumanne amesema pamoja na utaratibu huo kuwepo kisheria, pia unamsaidia mtoa huduma kuongeza uaminifu wa wateja kwa kampuni au mtu binafsi anayetoa huduma za usafirishaji wa bidhaa kwa sababu inathibitisha kuwa mtoaji huduma anafuata taratibu na kanuni za usalama za kusafirisha vifurushi na vipeto.

“Ili kutoa elimu zaidi tumeanzisha kampeni inayoitwa ‘Tuma Chap chap’ kwa usalama ambayo inalenga kuwaelimisha watumiaji wa huduma hizo kutumia watoa huduma waliosajiliwa na  kuwakumbusha watoa huduma kusajili huduma zao na kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo,”amesema.

Kwa upande wake mdau wa usafirishaji vifurushi na Meneja wa mabasi kampuni ya Galaxy, Magreth Kubiki amesema uwepo wa vitendo vya utapeli na udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya wasifirishaji wasio na leseni za kutoa huduma hiyo na wengine wakitumia majina ya kampuni mbalimbali zinazofanya shughuli hiyo imekuwa ni moja kati ya changamoto ambayo imekuwa ikiwakabili wanapokuwa wakitoa huduma hiyo.