TCRA yarejesha usajili wa maudhui mitandaoni

TCRA yarejesha usajili wa maudhui mitandaoni

Muktasari:

  • Siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza vyombo vya habari vilivyofungiwa na Serikali vifunguliwe, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeondoa zuio la utoaji wa leseni za huduma ya maudhui ya mtandaoni kuanzia jana Ijumaa ya Aprili 9, 2021.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza vyombo vya habari vilivyofungiwa na Serikali vifunguliwe, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeondoa zuio la utoaji wa leseni za huduma ya maudhui ya mtandaoni kuanzia jana Ijumaa ya Aprili 9, 2021.

Rais Samia alitoa agizo hilo Aprili 6 alipokuwa akiwaapisha baadhi ya makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu wa wizara mbalimbali katika Ikulu ya Dar es Salaam na akaitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa zikiwemo televisheni za mitandaoni.

TCRA ilisitisha kwa muda upokeaji wa maombi mapya na utoaji wa leseni za huduma za maudhui mitandaoni kuanzia Januari 28 na zuio hilo lilitakiwa kuishia Juni 30.

Taarifa ilitolewa jana na TCRA kwa vyombo vya habari ilisema mamlaka hiyo imeanza kupokea maombi ya leseni na watakaokidhi vigezo wataruhusiwa.

“TCRA inapenda kutoa taarifa kuwa, kuanzia leo Aprili 9 usitishwaji umeondolewa na TCRA imeanza kupokea maombi mapya ya leseni za maudhui ya mitandao,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi Digital, Ofisa mawasiliano wa TCRA Semu Mwakyanjala, amekiri kuwa taarifa hiyo ni ya kweli na wameitoa wao ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia.

“Mojawapo ya sababu ya kukuondoa zuio ni hiyo kauli ya Rais, kwa hiyo kazi inaendelea ya kusajili,” amesema Mwakyanjala.

Ameendelea, “Kuna kazi ya kitaalamu imefanyika ili kuhakikisha tunasimamia vyombo hivyo ndiyo maana tumeondoa zuio.”

Alipoulizwa kuhusu tozo za usajili wa maudhui a mitandaoni zinazolalamikiwa na wadau, Mwakyanjala alisema zitaendelea kuwa hivyo hivyo kwa kuwa zimewekwa kisheria.

“Zile tozo ni kwa mujibu wa sheria na kanuni, kwa hiyo itategemea Wizara itakavyoamua,” amesema.