TCRA yataka mfumo mmoja kusikiliza malalamiko ya wateja huduma za mtandaoni
Muktasari:
Imeelezwa kuwa kuna umuhimu taasisi zinazotoa huduma kupitia mitandao ya simu kuwa na mfumo rahisi wa kupokea malalamiko ya wateja linapotokea tatizo.
Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa kuna umuhimu taasisi zinazotoa huduma kupitia mitandao ya simu kuwa na mfumo rahisi wa kupokea malalamiko ya wateja linapotokea tatizo.
Hayo yameelezwa jana Jumatano Desemba 4, 2019 na mkuu wa kitengo cha usimamiaji na utekelezaji wa sheria wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Philip Filikunjombe katika kongamano la maadhimisho ya siku ya ushindani duniani.
Amesema mtu akinunua umeme, kuna taasisi zaidi ya tatu zinahusika na mteja akikosea huduma hiyo huanza kuhangaika kupiga simu katika maeneo yasiyohusika, ikiwemo TCRA.
Amesema utumaji fedha unahusisha benki, kwamba fedha inatakiwa kurudishwa kwa mteja saa kadhaa kama huduma imekosekana.
"Sheria hii inaonekana ngumu kutekelezeka kwa wahusika kwa sababu mtu anakaa hata zaidi ya siku tatu ndio anarudishiwa fedha kitu ambacho sio sahihi na wakati mwingine ukiuliza mitandao husika wanakuambia hela yako kuna mahali inashikiliwa, hii sio sawa.”
“Mbali na BoT (Benki Kuu Tanzania) katika utoaji huduma hii pia kuna kampuni iliyopewa kazi ya kukurudisha namba za Luku, kuna Tanesco na mtandao husika unaokukata hela, ukiangalia wote hawa walipaswa kuwa na utaratibu mmoja wa kupokea malalamiko ya mteja lakini haipo hivyo,” amesema Filikunjombe.
Amesema pamoja na biashara ya mtandao kufanya vizuri kwa sasa na kuwarahisishia watu maisha, kuna haja ya watumiaji kupewa elimu zaidi ili kuelewa vizuri sheria ya miamala ya kielektroniki.
Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC), Profesa Humphrey Moshi amesema teknolojia ya habari imewezesha biashara kufanyika bila mipaka ya nchi na biashara kati ya mataifa hufanyika kwa kasi kubwa.
"Kutokana na hilo tumeona ipo haja ya kuketi na taasisi za udhibiti kujadili changamoto mbalimbali na kutafuta njia ya kuzitatua ili wanaotumia huduma hiyo kuwa salama,” amesema mwenyekiti huyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCC, Dk John Mduma amesema maadhimisho ya siku ya ushindani duniani yalianza mwaka 1980 lakini kwa Tanzania yameanza mwaka 2015.
Dk Kaduma amesema kauli mbiu mwaka 2019 ni ‘kuhakikisha ushindani madhubuti katika ukuaji wa dunia ya kimtandao'.