TCRA yazifungia nyimbo 15, mbili za Diamond

Muktasari:

  • Katika taarifa ya mamlaka hiyo iliyotolewa leo Februari 28, 2018 inaeleza kuwa nyimbo hizo zilizotolewa na wasanii na kusambazwa katika vyombo mbalimbali vya utangazaji na mitandao ya kijamii, zina maudhui ambayo ni kinyume na maadili na kanuni za huduma za utangazaji.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesitisha kuchezwa kwa nyimbo 15 zisizokuwa na maadili, zikiwemo mbili za msanii Nassib Abdul maarufu Diamond.

Katika taarifa ya mamlaka hiyo iliyotolewa leo Februari 28, 2018 inaeleza kuwa nyimbo hizo zilizotolewa na wasanii na kusambazwa katika vyombo mbalimbali vya utangazaji na mitandao ya kijamii, zina maudhui ambayo ni kinyume na maadili na kanuni za huduma za utangazaji.

Hata hivyo, baadhi ya nyimbo hizo zimeshafungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), lakini baadhi ya televisheni na redio ziliendelea kuzicheza jambo ambalo Basata imefafanua kuwa wenye mamlaka ya kuzuia nyimbo hizo kupigwa katika vituo hivyo ni TCRA, si wao licha ya kuwa walizifungia

Mamlaka hiyo leo imetuma barua katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni kuvitaka kutozicheza nyimbo hizo.

Imezitaja nyimbo hizo kuwa ni Hallelujah na Wakawaka (Diamond), Kibamia (Roma Mkatoliki), Pale kati patamu na Maku makuz (Ney wa Mitego), Hainaga ushemeji wa Manifongo, I am Sorry JK (Nikki Mbishi).

Nyingine ni Chura na Nimevurugwa (Snura), Tema mate tumchape (Madee), Uzuri wako (Jux), Nampa papa (Gigy Money) na Nampaga (Baranaba),Nikono juu (Ney wa Mitego) na Bongo bahati mbaya wa Young Dee