TEC yataja sababu vifo mapadri 25, watawa 60

Wednesday March 03 2021

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima amesema zaidi ya mapadri 25, watawa zaidi ya 60 na wazee wawili wa  Baraza la Walei wamefariki dunia ndani ya miezi miwili kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo changamoto ya upumuaji.

Padri Kitima amesema hayo leo Jumatano Machi 3, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali hasa mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 akiwataka waumini wa kanisa hilo  kuendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali.

Makamu mkuu huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), amesema viongozi wa kiroho wamefariki dunia  katika  maeneo mbalimbali kati ya Desemba, 2020 hadi Februari 2021 .

"Naomba muendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa kwa kufuata maelekezo ya Wizara ya Afya. Mapadri wanakufa na masista wanakufa lakini hii ndani ya miezi miwili imetushtua sana hasa ukizingatia Serikali imeimarisha mifumo bora ya afya," amesema Kitima.

Amesema rais wa TEC, Gervas Nyaisonga amesambaza mwongozo kwa maaskofu wa majimbo mbalimbali kuhusu hatua za kuchukua kujikinga na maambukizi ya corona.

Advertisement
Advertisement