TEF: Tusitunge sheria kukomoana

Muktasari:

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema Tanzania haipaswi kutunga sheria ili kuwakomoa au kudhibiti wanahabari bali itunge kuwezesha ukuaji wa tasnia ya habari.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema Tanzania haipaswi kutunga sheria ili kuwakomoa au kudhibiti wanahabari bali itunge kuwezesha ukuaji wa tasnia ya habari.
Balile amesema sheria ikitungwa ili kudhibiti habari, huwa na matatizo yaliyojificha lakini ikiwa ni wezeshi, hutoa fursa ya kupata mawazo mapya yanayolenga ufanisi zaidi.
Mwenyekiti huyo ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi Agosti 6, 2022 jijini Dar es Salaam, wakati akazungumzia machakato wa mabadiliko ya sheria ya habari katika Kipindi cha Mezani kinachorushwa na Kituo cha Redio cha EFM.
 “Unapotunga sheria ya kuzuia ama kuminya habari, ujue kuna madhara makubwa unayatengeneza hapo mbele. Ndio maana tunazungumza na Serikali ili tuwe na sheria zinazokubalika kimataifa.
“Tusifurahie kutunga sheria mbaya kwa ajili ya kuumiza wengine, tusitunge sheria kwa ajili ya kukomoa waandishi bali tutafute ufanisi katika tasnia ya habari,” amesema.
Kwenye mahojiano hayo, Balile amesema duniani kuna namna tatu za kusimamia vyombo vya habari na kila nchi hutumia moja kati ya hizo kulingana na matakwa ya watawala.
“Kuna mfumo wa kwanza ni self regulation (kujitathmini), mfumo wa pili ni Serikali ‘kushika’ vyombo vya habari kama ilivyo sasa na mfumo wa tatu ni co-regulation ambapo Serikali na wadau wa habari wanakuwa na chombo ambacho kinawaunganisha.
“Sisi tunataka huu mfumo wa tatu ambao ndio tunaupigania, sio ule wa Serikali kuwa mlalamikaji, msuluhishi na hakimu. Huu mfumo utazikwa kwa kuunda Baraza la Huru la Vyombo vya Habari,” amesema Balile.  
Akizungumzia ushirikishwaji wa wanahabari wenyewe kwenye mabadiliko hayo, Balile amesema wamekuwa na mikutano ya mara kwa mara na wanahabari katika kuwafafanulia vifungu hivyo.
Ameongeza kuwa TEF imekuwa ikifanya mikutano na wahariri, waandishi pamoja na waandishi wa habari za mtandaoni (online contents).
“Vikao hivi tumevifanya mara kwa mara na waandishi wanaelewa, na hatua iliyopo sasa ni kwenda kwenye mjadala ulioitishwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Agosti 11 – 12, mwaka huu kwa ajili ya kupitia vifungu vinavyolalamiukiwa,” amesema.
Akijibu swali kuhusu TEF kufanya kazi kwa masilahi binafsi ya viongozi wake, Balile ameeleza kuwa, kwa mwaka mmoja aliokaa madarakani, kuna mafanikio yanayoonekana wazi .
Ametaja mafanikio hayo kuwa ni kushawishi tasnia ya habari kuhamishiwa katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ambapo sasa inaitwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Awali tasnia ya habari ilikuwa imeunganishwa na Michezo na Utamaduni.
Ameeleza kuwa, kanuni za ada kwa wamiliki wa televisheni walipaswa kulipa ada ya Sh70 milioni lakini TEF na wadau wamefanikisha kuzungumza na Serikali na kisha kushusha ada hiyo na kuwa Sh30 milioni.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kurejeshwa kwa channeli za televisheni za bure kwenye ving’amuzi vyote ambapo awali zilipelekwa kwenye vifurushi vya kulipia.
Ametaja mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya TEF ya sasa.
“Yote haya sidhani kama yanalenga masilahi binafsi, ukumbuke haya tumeyafanya ndani ya mwaka mmoja, hivyo nadhani mtu anayesema kuwa TEF ya sasa imejielekeza kwenye masilahi binafsi, afikiri upya kauli yake,” amesema.