TEF wataka kifungo kwa viongozi wasiolipa

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile

Muktasari:

  • Wakati vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini vikipiga miayo ya njaa kutokana na kutolipwa fedha zinazotokana na matangazo waliyoyatoa kwa Serikali Jukwaa la Wahariri Tanzania limetaka kuwepo na sheria ya kulazimisha malipo na vifungo kwa wanaokaidi.

Dar es Salaam. Wakati vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini vikipiga miayo ya njaa kutokana na kutolipwa fedha zinazotokana na matangazo waliyoyatoa kwa Serikali Jukwaa la Wahariri Tanzania limetaka kuwepo na sheria ya kulazimisha malipo na vifungo kwa wanaokaidi.

Mpaka sasa vyombo vya habari binafsi, vinadai Serikali fedha za matangazo zaidi ya Sh7.8 bilioni hali inayoviweka kwenye hali ngumu ya kujiendesha vyombo hivyo.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, wakati akifanya mahojiano na chombo kimoja cha habari juu ya mapendekesho ya sheria ya huduma za habari.

Balile alisema moja ya jambo muhimu katika mapendekezo ya mabadiliko ya sheria za habari, ni kuweka sheria walau pale taasisi ama wizara za Serikali zisipolipa fedha za matangazo, kiongozi wake afungwe walau miezi sita hivi.

Balile alisema, taasisi za Serikali zinadaiwa fedha nyingi na vyombo vya habari lakini hawalipi, hivyo kuundwa kwa sheria ya kuwabana wasipolipa watafungwa, itaongeza msukumo.

“Agosti leo na kesho tuna na mkutano wa wadau wa habari, hatuendi kushikana mashati na Serikali bali tunakwenda kupigania masilahi ya wanahabari na vyombo vyao.

Kiongozi huyo wa TEF alisema, vyombo vya habari kama ilivyo uwekezaji katika maeneo mengine, vinahitaji mtaji na biashara kubwa ni matangazo.

“Wanaposhindwa kulipa matangazo, maana yake wanasababisha shida kwenye vyombo vya Habari maana ili viendeshwe vinahitaji fedha, Sh7.8 bilioni ni nyingi sana.

“Hapo kuna mishahara ya waaandishi, wafanyakazi wa sekta nyingine kwenye vyombo vya habari, kuna fedha za uchapaji lakini pia matumizi ya ofisi, fedha hizi zisipolipwa ofisi zitaendeshwaje?,” alisema Balile.

Alisema, jambo hilo alimueleza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kutoa maelekezo kwa taasisi za Serikali kulipa madeni hayo pamoja na maelezo ya Waziri Mkuu, taasisi za Serikali hazijatekeleza.

 “Sasa kwenye mkutano huo, mambo kama haya tutazungumzia na ndio maana tunataka kuwe na sheria za namna hii, ili kulinda maslahi ya waandishi na uhai wa vyombo vya habari nchini,” amesema Balile.

Alisema, wanahabari wamekuwa wakiwajibika kwa namna utaratibu unavyoelekeza na ndio maana vyombo vya Habari vinatumika kupeperusha matangazo, lakini wajibu wa baadhi ya taasisi hautekelezwi.

“Sasa katika mabadiliko haya, suala la malipo ya matangazo liwekwe kisheria, atakayekaidi ajue kwamba ipo sheria na atawajibika kwayo,” alisema Balile.

Mwisho.