Tembo wavamia mashamba Mtwara

Muktasari:

  • Tembo wamezua hofu kwa wakazi wa Kata za Mahurunga na Tangazo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara baada ya kuharibu mazao yao na kuanza kuvunja mikorosho mashambani.

Mtwara. Tembo wamezua hofu kwa wakazi wa kata za Mahurunga na Tangazo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara baada ya kuharibu mazao yao na kuanza kuvunja mikorosho mashambani.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 20, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Selemani Nampanye amesema kuwa wamevamia mashamba ya korosho na kuvunja miti.

“Tembo wamemaliza haribu kundi, mboga za majani zote, nyanya, mahindi na sasa wamehamia kwenye mikorosho yaani wanaivunja vunja.

“Hofu yetu iko kwemye msimu wa maembe tunahofia watafika majumbani kwakuwa miembe iko hadi kwenye makazi ya watu,” amesema Nampanye.

Hivi karibuni Mfuko wa Kimataifa wa Mazingira (WWF) unefanya kikao mkoani Mtwara na kujumuisha Wakurugenzi wa Halmashauri za mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na  maofisa maliasili, Tawa, Tanapa na PAC ili kujadili suala la uvamizi wa tembo.

Akizungumzia mkakati wa kudhibiti wanyama, Ofisa mhifadhi wa WWF, Deogratius Kilasara amesema kuwa shirika hilo limekuja na mbinu ya kuwadhibiti tembo kwenda kwenye makazi ya watu kwa kuwafunga kifaa maalum kiitwacho Colla.

“Kazi ya kuwafunga Collas itawezesha kuwafuatilia na kugundua mienendo yao wakiwa ndani na nje ya hifadhi ambapo itatupa nafasi ya kuweza kuwafatilia kwa ukaribu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya alisema kuwa changamoto za tembo zimekuwa kubwa hasa katika kata Saba za Wilaya ya Mtwara ambazo ni Kitaya, Namtumbuka, Tangazo, Mahutunga, Mnongodi, Kiromba na Kitaya.